Jumamosi, 13 Aprili 2026 · Dar es Salaam, Tanzania
|
kijijichetumedia.com
Kijiji cha Habari Media
Kijiji cha Habari Media Simulizi za Mageuzi · SDGs · Tanzania
LEO
Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •    Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •   

Jumatatu, 14 Septemba 2026

Roboti zinaomba ‘tips’; fedha hizo zinaenda kwa nani?


Roboti Eunice

Kasi ya matumizi ya teknolojia katika sekta ya huduma, imekuja na changamoto mpya. Roboti zinazotengeneza kahawa na kupeleka chakula mezani zimeanza kuwaomba wateja malipo ya ziada yaani tips.

Swali kubwa linabaki kuwa fedha hizo zinawanufaisha wafanyakazi au kampuni zinazomiliki roboti? Watu wanahoji, nani anayestahili kupokea malipo ya ziada kutoka kwa wateja.

Ripoti za kimataifa zinaonesha kwamba kumekuwa na ongezeko la matumizi ya roboti katika sekta ya huduma, sehemu mbalimbali duniani hususani nchi zilizoendelea.

Katika The Tipsy Robot mjini Las Vegas, Marekani, kwa mfano, mikono ya roboti hutengeneza vinywaji, huku wateja wakitozwa pia ada ya huduma ya asilimia 10. Wakati huo huo, Artly Coffee, inayotumia roboti kutengeneza kahawa, imewahi kuwaomba wateja kutoa ‘tips’, ingawa baadaye iliondoa mfumo huo kufuatia malalamiko ya wateja.

Wataalamu wanasema mwitikio wa mteja aliyeombwa ‘tip’ ndio utakaoamua mustakabali wa sekta ya huduma.

Katika baa iitwayo The Tipsy Robot, mikono miwili ya roboti inayotengeneza vinywaji kwa njia ya kiotomatiki. Mteja anachokifanya ni kuchagua kile anachopendelea kwenye mfumo mahali hapo, kisha mikono miwili ya roboti inafanya kazi.

Mteja mmoja katika baa hiyo anasema alichagua ‘margarita’ na kushuhudia roboti ikichanganya tequila, maji ya limau na triple sec ambazo zilizunguka-zunguka kwa mbwembwe zisizo za lazima, kisha zikainama na kumkabidhi glasi.

“Kinywaji hicho kiligharimu Dola za Marekani 17 (takribani Sh. 45,000), lakini niligundua gharama nyingine ya ziada; ada ya huduma ya asilimia 10. Tipsy Robot ilitaka pia malipo ya ziada.

“Haikuwa mara yangu ya kwanza kukutana na hali hiyo. Roboti inayotengeneza kahawa katika Artly Coffee jijini New York pia iliniomba nitoe malipo ya ziada. Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Newark Liberty, mashine ya kujihudumia ilinipendekezea nitoe malipo ya ziada niliponunua chupa ya maji katika kibanda kisichokuwa na mhudumu.

Huko Portland, Oregon, nilihudumiwa na binadamu katika mkahawa wa Top Burmese, lakini chakula changu kililetwa mezani na roboti iliyokuwa ikijizungusha kwa magurudumu,” wanasema wateja tofauti.

“Kwa mhudumu binadamu, nilitoa kwa furaha malipo ya ziada ya asilimia 20, lakini katika matukio mengine nilisita. Kanuni za kutoa malipo ya ziada zinapoteza mwelekeo roboti zinaponyosha mikono yao ya kidijitali, na mara nyingi haijulikani ni nani anayezichukua fedha hizo,” anasema mteja mmoja.

Wawakilishi wa The Tipsy Robot na Artly Coffee wanasema wafanyakazi wao wote binadamu hugawana malipo yote ya ziada na kampuni hazipati chochote. Aidha, Artly imezima mfumo wa kuwaomba wateja malipo ya ziada tangu nilipotembelea.

“Tunayo kila sababu ya kuamini kwamba baadhi ya waajiri wasio waaminifu wanachukua wenyewe fedha zinazotolewa kwa roboti,” anasema Holona Ochs, profesa msaidizi wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Lehigh nchini Marekani na mwandishi mwenza wa kitabu Gratuity.

“Swali muhimu ni nani anayenufaika na nani anayelipa gharama,” anasema Ochs.

Tangu janga la COVID-19, watu wamekuwa wakiombwa kutoa malipo ya ziada katika maeneo mengi zaidi kuliko hapo awali, mara nyingi kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali.

Unapompa mfanyakazi nchini Marekani malipo ya ziada, sheria inasema kampuni, wamiliki na wasimamizi hawawezi kuchukua sehemu ya fedha hizo. Lakini unapolipa roboti, huenda kukawa na mwanya wa kisheria.

“Bado hakuna kiwango cha kisheria kilichowekwa kinachoeleza nani anamiliki malipo yanayotolewa kwa roboti,” anasema Ochs.

Anasema utawala wa Rais Donald Trump umefanya iwe vigumu zaidi kwa wafanyakazi kufuatilia madai yanayohusiana na matatizo ya malipo ya ziada, huku baadhi yao wakificha simulizi zao kwa kuhofia kulipiziwa kisasi.

“Kwa hiyo, ikiwa waajiri wanachukua malipo yanayotolewa kwa roboti, kwa sasa tuna njia chache sana za kujua,” anasema.

“Mara nyingi unaweza kuwaona watu wakifanya kazi jikoni au nyuma ya baa, lakini huenda fedha za malipo ya ziada zinaenda kwa kampuni. Hakuna kanuni.”

Hata hivyo, hilo halimaanishi kwamba mashine za kiotomatiki ni mbaya kwa wafanyakazi wa sekta ya huduma.

Kivutio cha roboti ndicho kinachowafanya watu kutembelea maeneo kama Tipsy Robot na Artly Coffee. Kwa hiyo, wafanyakazi wanaofanya kazi pamoja na mashine hizo huenda wasingekuwa na ajira hizo kama roboti zisingekuwepo.

Artly inasema uamuzi wake wa kuzima mfumo wa kuomba malipo ya ziada na kuongeza mishahara ya wafanyakazi ulitokana kwa sehemu na malalamiko ya wateja kuhusu utaratibu huo.

Baadhi ya matawi sasa yana vibakuli vya kawaida vya kuweka malipo ya ziada, lakini asilimia 100 ya fedha hizo bado huenda kwa wafanyakazi binadamu, anasema Abigail Smathers, mkurugenzi wa maudhui katika Artly.

“Hatuna imani na kutumia teknolojia kwa lengo la kupunguza gharama kwa gharama ya binadamu,” anasema.

Smathers anasema kuna uhaba wa wafanyakazi katika sekta ya huduma na kwamba roboti zinaweza kusaidia bila kuwaondoa binadamu kwenye ajira.

Hata hivyo, anakiri kwamba akili mnemba (AI), inatumika katika maeneo ambayo huenda haikupaswa kutumika.

“Lakini mwisho wa siku, hapo ndipo tatizo lilipo. Teknolojia hii si ovu kwa asili. Maadili yake yanategemea nia na namna inavyotekelezwa,” anasema.

“Tunafanya kila tuwezalo kujenga kwa nia njema, kutenda kwa uadilifu na kuhakikisha kwamba mustakabali wa teknolojia hii unawanufaisha wengi, si wachache.”

Katerina Berezina, profesa msaidizi anayefanya utafiti kuhusu teknolojia katika sekta ya ukarimu katika Chuo Kikuu cha Mississippi, Marekani, anasema sekta hiyo inastahili kupewa pongezi zaidi.

“Sidhani kama ni haki kudhani kwamba haya ni makampuni yanayojaribu tu kupata fedha kwa gharama yoyote,” anasema.

“Ada ya ziada au ada ya huduma inaweza kuwa tu njia ya kugharamia kazi muhimu au masasisho ambayo roboti inahitaji.”

Anasema kutoa malipo ya ziada ni jambo la kawaida katika sekta hiyo na kwamba kampuni zinafanya kazi ndani ya mazingira yaliyowekwa na soko.

Kwa upande mwingine, baadhi ya mashirika, likiwemo One Fair Wage, yanasema matumizi ya roboti ni juhudi nyingine ya kuendeleza malipo duni, ambayo ndiyo chanzo halisi cha uhaba wa wafanyakazi katika migahawa.

Bila kujali uzito wa sababu mbalimbali zinazohusika, wataalamu wanasema mustakabali wa jambo hili utategemea namna wewe na wateja wengine mtakavyoitikia majaribio tunayoyaona sasa.

Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani na mwandishi wa kitabu The Psychology of Tipping, Michael Lynn, anataka watu wafikirie sababu za kutoa au kutokutoa tips.

“Fikiria sababu kuu zinazotufanya tutoe malipo ya ziada,” anasema akisisitiza kwamba watu hutoa malipo ya ziada ili kuthamini huduma nzuri au kwa sababu za kujitolea, kwa lengo la kusaidia kuongeza kipato cha wafanyakazi wanaolipwa mishahara midogo.

Anasema kwa upande wa roboti, hakuna sababu ya kufanya hivyo.

Katika utafiti mmoja, ni takribani asilimia 11 tu ya washiriki waliosema wangekuwa tayari kutoa malipo ya ziada kwa mhudumu wa baa ambaye ni roboti.

“Lakini watu ambao walikuwa na uzoefu wa moja kwa moja na wahudumu wa baa wa roboti walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa tayari kutoa malipo ya ziada kuliko watu wengine,” anasema Berezina, ambaye alikuwa mmoja wa waandishi wa utafiti huo.

Na ingawa watu wengi walisema hawatatoa malipo ya ziada kwa roboti, takribani asilimia 42 walibadili mawazo yao walipoambiwa kwamba fedha hizo zingeenda kwa wafanyakazi binadamu.

Prof. Lynn anasema biashara zinaanzisha mfumo wa roboti kuomba malipo ya ziada kwa sababu unasaidia kuongeza mapato na kwamba utawafukuza wateja kuondoka, huenda ukafa.

Roboti Eunice alipotambulishwa bungeni na aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

 Chanzo: BBC

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni