Jumamosi, 13 Aprili 2026 · Dar es Salaam, Tanzania
|
kijijichetumedia.com
Kijiji cha Habari Media
Kijiji cha Habari Media Simulizi za Mageuzi · SDGs · Tanzania
LEO
Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •    Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •   

Ijumaa, 18 Septemba 2026

INTERPOL yatumia AI kuwatambua washukiwa 126 wa ugaidi

Maofisa wa INTERPOL wakiwa kazini. PICHA: INTERPOL

 Operesheni ya kwanza ya aina yake inayolenga kuvuruga mitandao ya kigaidi katika anga ya kidijitali, imetumia Akili Mnemba (AI), kubaini watu 126 wanaoshukiwa kujihusisha na ugaidi.

Wamebainika baada ya Shirika la Kimataifa la Polisi wa Uhalifu (INTERPOL), kuendesha Operesheni Shams II, iliyowahusisha maofisa na wataalamu waliobobea kutoka nchi 11, waliotoa picha za nyuso 108,076 kutoka kwenye maudhui ya picha na video yaliyochapishwa na makundi ya kijihadi.

Maofisa hao walitumia mawakala wa AI waliopangiliwa pamoja na misimbo ya hali ya juu iliyozalishwa na AI kukusanya taarifa na kupunguza idadi hiyo hadi kufikia picha 6,362 za nyuso za kipekee, ambazo zilikuwa tayari kuchakatwa kupitia Mfumo wa INTERPOL wa utambuzi wa nyuso.

Taarifa ya INTERPOL iliyotolewa leo Septemba 18, 2026 imesema matokeo yaliyotolewa na AI yalifanyiwa mapitio na uhakiki na maofisa na wachambuzi waliopewa mafunzo, kwa kuzingatia kanuni za shirika hilo kuhusu uchakataji wa taarifa.

“Operesheni Shams II, iliyofanyika kuanzia Juni 1 hadi 5, 2026 na kuratibiwa na INTERPOL, iliwakutanisha maofisa na wataalamu 28 waliobobea kutoka nchi 11.

“Katika siku tano za operesheni hiyo iliyofanyika kwa uratibu mjini Tunis, Tunisia, maofisa wa vyombo vya sheria walitoa picha 108,076 za nyuso kutoka kwenye maudhui ya picha na video yaliyochapishwa na makundi ya kijihadi.

“Teknolojia hiyo iliwezesha mfumo kuondoa picha zilizojirudia na kukagua ubora wa picha, na hivyo kupunguza mkusanyiko wa data hadi kufikia picha 6,362 za nyuso, zilizokuwa tayari kuchakatwa kupitia mfumo wa INTERPOL wa utambuzi wa nyuso,” imesema taarifa ya shirika hilo.

Taarifa hiyo imesema mbali na picha zilizopatikana kutoka kwenye majukwaa ya mtandaoni, maofisa kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Kati ya INTERPOL mjini Baghdad, Iraq, walitoa mkusanyiko mkubwa wa taarifa za kiintelijensia zinazohusiana na washukiwa wa ugaidi.

“Hadi sasa, Wapiganaji 126 wa Kigeni wa Kigaidi (Foreign Terrorist Fighters), wametambuliwa kutokana na picha zilizochakatwa wakati wa Operesheni Shams II. Ulinganisho huo utaimarisha taarifa zilizopo kuhusu washukiwa, ikiwa ni pamoja na kubaini maeneo wanayoweza kuwa na mitandao yao ya kijamii.

“Taarifa hizo sasa zinaunganishwa katika kanzidata za INTERPOL, hatua inayolenga kuimarisha juhudi za kimataifa za kubaini, kufuatilia na kuvuruga harakati za kigaidi duniani,” imefafanua.

INTERPOL imesema taarifa muhimu zilizopatikana wakati wa uchunguzi huo zinatumika kusaidia taratibu za kisheria katika nchi zilizoshiriki, ikiwa ni pamoja na kesi moja inayowahusu washukiwa wawili wa Wapiganaji wa Kigeni wa Kigaidi ambao kwa sasa wamezuiliwa.

“Kwa kuwa bado kuna maelfu ya picha ambazo hazijachakatwa, ulinganishaji zaidi unaendelea na unaweza kusaidia kubaini taarifa nyingine muhimu kwa uchunguzi,” imesema.

Mbali ya picha hizo, INTERPOL imesema Operesheni Shams II pia ilitumia zana za kisasa za uchunguzi wa miamala ya sarafu za kidijitali (cryptocurrency), kufuatilia fedha zinazotumika kinyume cha sheria.

Hatua hiyo ilisababisha kutumwa kwa maombi matatu ya dharura kwa Watoa Huduma za Mali za Mtandaoni (Virtual Asset Service Providers), ili kutoa taarifa za wateja, kwa lengo la kuvuruga mtiririko wa fedha unaofadhili ugaidi.

Aidha, shirika hilo limesema mbali na shughuli za uchunguzi, nchi zilizoshiriki zilikutana pia na wawakilishi wa sekta ya michezo ya mtandaoni kujadili suala la vijana kuingizwa katika misimamo mikali kupitia mazingira ya mtandaoni.

Mkurugenzi wa INTERPOL anayeshughulikia Kukabiliana na Ugaidi, María Carmen Muñoz González, amesema: “Mafanikio ya Operesheni Shams II yanaonesha umuhimu wa kuunganisha ushirikiano wa kimataifa wa vyombo vya sheria na uwezo wa uchanganuzi unaosaidiwa na AI kwa matumizi yanayowajibika.

Mtindo huu wa kiutendaji unatoa msingi imara wa kusaidia ushirikiano wa baadaye wa kimataifa wa vyombo vya sheria katika kuwalenga wahusika wa uhalifu duniani.”

Operesheni Shams II ilitekelezwa chini ya Mradi wa CT TECH+, unaofadhiliwa na Vyombo vya Umoja wa Ulaya vya Sera za Nje (European Union’s Foreign Policy Instruments) na kuungwa mkono na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Ugaidi (UNOCT).

Nchi zilizoshiriki operesheni hiyo ni Côte d’Ivoire, Ghana, Iraq, Kenya, Malaysia, Nigeria, Ufilipino, Qatar, Tajikistan, Tunisia na Uzbekistan.

CHANZO: INTERPOL

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni