Mfumo wa Akili Bandia (AI) umebaini kila mjamzito aliye katika hatari kubwa ya kupata shinikizo la damu linalotokana na ujauzito (Hypertensive Disorders of Pregnancy – HDP), ambalo ni miongoni mwa sababu kuu za vifo vya akina mama nchini Tanzania.
Matokeo hayo yanatoa matumaini kwamba teknolojia hiyo
inaweza kusaidia kupunguza vifo vya wajawazito, kwa kuwezesha wahudumu wa afya
kuwabaini mapema walio katika hatari na kuwapatia huduma stahiki kabla hali zao
hazijawa mbaya.
Utafiti huo ulibaini kuwa modeli bora zaidi ya
ujifunzaji wa mashine (machine learning), ilifikia usahihi wa asilimia 90.1 na
uwezo wa asilimia 100 wa kuwabaini wajawazito wote waliokuwa katika hatari
kubwa wakati wa utafiti.
Watafiti wanasema mfumo huo uliwatambua wanawake
12,603 kuwa katika hatari kubwa, wakiwemo baadhi ambao wangeweza kupuuzwa
katika tathmini za kawaida za kliniki ya wajawazito.
Matokeo hayo, yaliyochapishwa hivi karibuni katika
jarida la PLOS Digital Health, yanaonesha kuwa AI inaweza kuimarisha
huduma za kliniki ya wajawazito kwa kuwasaidia wahudumu wa afya kubaini mapema
wanawake walio katika mazingira hatarishi kabla ya kupata madhara makubwa.
Wanasayansi hao wanasema AI inaweza kufaa zaidi katika
maeneo yenye uhaba wa rasilimali ambapo wahudumu wa afya hukabiliwa na idadi
kubwa ya wagonjwa na muda mfupi wa kufanya tathmini za kina kwa kila mgonjwa.
Utafiti huo uliongozwa na Dk. Isaac Lyatuu kutoka Prime
Health Initiative Tanzania na Taasisi ya Afya ya Ifakara (Ifakara Health
Institute), kwa ushirikiano na Emmanuel Mwanga na Alen Kinyina kutoka taasisi
hiyo. Pia ulihusisha watafiti na wataalamu wa afya ya umma kutoka Wizara ya
Afya, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Sekretarieti ya Mkoa wa Geita pamoja na Prime Health Initiative Tanzania.
Ili kupima uwezo wa mfumo huo, watafiti walichambua
kumbukumbu 337,027 za huduma za kliniki ya wajawazito zilizokusanywa kupitia
Mfumo wa Umoja wa Jamii (Unified Community System – UCS), kati ya mwaka 2023 na
2024. Taarifa hizo ziliwakilisha wajawazito 187,438 waliopata huduma katika
vituo vya afya vilivyopo katika mikoa 23 nchini.
Katika utafiti huo, modeli tano za ujifunzaji wa
mashine zilifanyiwa tathmini, ili kubaini mfumo wenye uwezo mkubwa zaidi wa
kutabiri hatari ya shinikizo la damu la ujauzito.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, modeli iliyojulikana kama
Extreme Gradient Boosting (XGBoost), ndiyo iliyofanya vizuri zaidi.
Ilipofanyiwa majaribio kwa kutumia seti nyingine huru ya taarifa zenye zaidi ya
kumbukumbu 120,000 za wagonjwa, ilifikia usahihi wa asilimia 90.1 pamoja na
alama ya Area Under the Curve (AUC) ya 0.95, kiwango kinachoonesha uwezo mkubwa
wa kutabiri kwa usahihi.
Wanasayansi hao wanasema modeli hiyo iliweza kuwabaini
wanawake wote waliokuwa katika hatari kubwa waliokuwamo kwenye seti ya
kuthibitisha matokeo.
"Mfumo huu wenye uwezo mkubwa wa kubaini walio
katika hatari huwatambua pia baadhi ya wagonjwa ambao baadaye hawapati matatizo
hayo, unafanya kazi kama kinga madhubuti ya usalama.
“Kwa kuendesha mchakato wa kubaini hatari mapema,
vituo vya kutolea huduma za afya vinaweza kuongeza kwa kiwango kikubwa ufanisi
wa utoaji huduma na kuhakikisha kuwa madaktari bingwa na wataalamu wengine
wenye majukumu mengi wanatumia muda wao mchache kuwahudumia wagonjwa
wanaouhitaji zaidi," watafiti waliandika, wakieleza kuwa madhara ya
kushindwa kumtambua mwanamke ambaye baadaye atapata matatizo makubwa ni makubwa
zaidi kuliko kufanya uchunguzi wa ziada kwa wanawake ambao baadaye hubainika
kutokuwa katika hatari.
Utafiti huo pia uliangazia changamoto zinazokabili
utoaji wa huduma za kliniki ya wajawazito nchini Tanzania. Ingawa Shirika la
Afya Duniani (WHO) linapendekeza wajawazito kuhudhuria angalau kliniki mara nane
katika kipindi cha ujauzito, ni wanawake 157 pekee (sawa na asilimia 0.08), ya
washiriki wote wa utafiti waliokamilisha mahudhurio hayo. Zaidi ya nusu ya
wanawake wote walikuwa na kumbukumbu ya kuhudhuria kliniki moja pekee ya
kliniki, huku chini ya nusu wakihudhuria mara mbili au zaidi.
Watafiti wanasema matokeo hayo yanaonesha umuhimu wa
kuwa na zana zinazoweza kufanya tathmini sahihi ya hatari hata pale taarifa za
mgonjwa zinapokuwa chache.
Waandishi wa utafiti huo wanasisitiza kuwa mfumo wa AI
umekusudiwa kuwasaidia wataalamu wa afya kwa kuwa unawabaini mapema wanawake
wanaohitaji uangalizi wa karibu kabla ya kuonana na daktari au mtoa huduma huku
ikiboresha mtiririko wa wagonjwa katika vituo vya afya na kuhakikisha
rasilimali chache za kibingwa zinaelekezwa kwa wagonjwa wanaohitaji zaidi.
Watafiti hao wanasema matokeo hayo yanathibitisha kuwa
taarifa za kidijitali zinazokusanywa katika huduma za kawaida za afya zinaweza
kutumika kuendesha mifumo ya AI kutathmini hatari katika ngazi ya huduma za
msingi. Wanaamini kuwa mfumo huo unaweza kuongeza ufanisi wa huduma za kliniki
ya wajawazito na kuimarisha juhudi za kupunguza vifo vya akina mama vinavyoweza
kuzuilika.
Hata hivyo, walionya kuwa kiwango cha mfumo kuwatambua
baadhi ya wanawake wasiokuwa na tatizo kuwa katika hatari ni kikubwa kiasi,
hivyo unapaswa kutumika kama chombo cha kupanga kipaumbele cha uchunguzi wa
wagonjwa, badala ya kuwa mfumo wa kutoa utambuzi wa mwisho wa ugonjwa. Wanapendekeza
kuwa watakaobainishwa kuwa katika hatari wanapaswa kufanyiwa vipimo vya ziada
vya gharama nafuu kabla ya kufikiwa uamuzi wa kitabibu.
Kadhalika, watafiti wanapendekeza Wizara ya Afya
kuwekeza zaidi katika kuunganisha mifumo ya kidijitali ya taarifa za afya,
kuboresha ubora wa taarifa zinazokusanywa katika vituo vya afya, na kutekeleza
majaribio ya hatua kwa hatua ili kutathmini athari za teknolojia hiyo katika
huduma za afya, mahitaji ya rasilimali, ufanisi wa utekelezaji na usawa kabla
ya kuisambaza nchini kote.
Iwapo mfumo huo utaunganishwa kwa mafanikio katika
miundombinu ya kidijitali ya afya inayopanuka nchini Tanzania, watafiti
wanasema teknolojia ya AI inaweza kupunguza mzigo wa mojawapo ya visababishi
vikuu vya vifo vya akina mama nchini.
Taarifa zinaonesha kwamba shinikizo la damu la
ujauzito linaendelea kuwa mojawapo ya changamoto kubwa za afya ya uzazi nchini
Tanzania. Inakadiriwa kuwa huathiri kati ya asilimia tano hadi 10 ya wajawazito
na kuchangia takribani asilimia 34 ya vifo vya moja kwa moja vinavyotokana na
matatizo ya uzazi.
Aidha, taarifa zinaonesha kwamba licha ya uwepo wa
huduma za kliniki ya wajawazito, wanawake wengi hugundulika wakiwa tayari
katika hatua za mwisho za ugonjwa kutokana na vituo vingi vya afya kutegemea
kipimo kimoja cha shinikizo la damu wakati wa mahudhurio ya kawaida ya kliniki.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni