![]() |
| Mwanasayansi, Deogratius Kavishe |
UTAFITI mpya uliofanyika vijijini nchini Zambia umebaini kuwa kunyunyiza viuatilifu tofauti katika nyumba zinazopakana, kunaweza kusaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu huku ukiendelea kutoa kinga dhidi ya malaria.
Utafiti huo uliochapishwa Mei 17, 2026 katika jarida
la Medical and Veterinary Entomology, ulijaribu mbinu ya kunyunyizia viuatilifu
katika kiwango cha kaya inayojulikana kama “micro-mosaic”.
Badala ya kutumia aina moja ya kiuatilifu katika jamii
nzima, watafiti walitumia viuatilifu tofauti kwa kupishana katika nyumba
jirani. Lengo la mbinu hiyo ni kukabiliana na moja ya changamoto kubwa
zinazozikabili programu za kudhibiti malaria kwa sasa—kuongezeka kwa usugu wa
mbu dhidi ya viuatilifu vinavyotumika kwa kawaida.
Watafiti waliohusika katika utafiti huo ni Dingani
Chinula, Kenzo Mumba, Reuben Zulu, Ketty Ndhlovu, Deogratius Kavishe, Neil
Philip Hobbs, Samson Kiware, Thomas Reed, Busiku Hamainza na Gerry F. Killeen.
Timu hiyo ilijumuisha wanasayansi kutoka Zambia, Tanzania, Ireland na
Uingereza, akiwemo wataalamu kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI).
Usugu wa viuatilifu ni tishio linaloongezeka
Kwa mujibu wa watafiti, usugu wa mbu kwa viuatilifu ni
moja ya vitisho vikubwa vinavyoweza kudhoofisha mafanikio yaliyopatikana katika
mapambano dhidi ya malaria barani Afrika.
Wanasema mbu wanapoendelea kukutana mara kwa mara na
kiuatilifu kilekile, wale wenye uwezo wa kustahimili kemikali hizo huwa na
nafasi kubwa ya kuishi na kurithisha sifa hizo kwa vizazi vijavyo. Hali hiyo
husababisha viuatilifu kupoteza ufanisi wake taratibu.
Katika utafiti huo, watafiti walilinganisha mikakati
mitatu ya upuliziaji wa ndani ya nyumba (Indoor Residual Spraying – IRS), mbinu
inayohusisha kunyunyizia viuatilifu kwenye kuta za ndani za nyumba ambako mbu
hupumzika baada ya kunyonya damu.
Mikakati hiyo ilijumuisha matumizi ya DDT pekee,
matumizi ya mchanganyiko wa clothianidin na deltamethrin pekee, na mfumo wa
“micro-mosaic” uliotumia viuatilifu hivyo viwili kwa kupishana kati ya nyumba
jirani.
Utafiti ulifanyikaje?
Utafiti ulifanyika katika Wilaya ya Luangwa, Kusini
Mashariki mwa Zambia, ambapo watafiti walifuatilia idadi ya mbu katika kaya 135
zilizogawanywa katika maeneo tisa ya vituo vya afya kwa kipindi cha mwaka mmoja
baada ya kampeni ya kawaida ya IRS.
Nyumba hizo ziligawanywa katika makundi matatu ya
majaribio. Kundi la kwanza lilinyunyiziwa DDT pekee, kundi la pili
lilinyunyiziwa mchanganyiko wa clothianidin na deltamethrin, huku kundi la tatu
likitumia mfumo wa “micro-mosaic” ambapo nyumba moja ilinyunyiziwa DDT na
nyumba inayofuata ilinyunyiziwa mchanganyiko wa clothianidin na deltamethrin.
Katika kipindi cha utafiti, watafiti walifanya jumla
ya usiku 1,620 wa kunasa mbu kwa kutumia mitego maalumu ya kisayansi.
Matokeo yalionyesha nini?
Matokeo yalionyesha kuwa idadi ya mbu wanaosambaza
malaria ilikuwa ndogo katika makundi yote matatu ya utafiti.
Watafiti hawakubaini tofauti kubwa katika msongamano
wa mbu wala aina za mbu waliokutwa chini ya mikakati yote mitatu ya upuliziaji.
“Matokeo hayo yanaashiria kuwa mbinu ya ‘micro-mosaic’
katika kiwango cha kaya inaweza kutoa kinga dhidi ya mbu wa malaria
inayolingana na ile ya mbinu za kawaida za upuliziaji, huku ikitoa fursa ya
ziada ya kudhibiti usugu wa viuatilifu,” imeeleza ripoti ya utafiti huo.
Aidha, watafiti walibaini kuwa utekelezaji wa mfumo
huo ulikuwa rahisi na unaowezekana katika mazingira ya kawaida ya programu za
kudhibiti malaria.
Fursa mpya katika mapambano dhidi ya malaria
Kwa mujibu wa watafiti, kuwakabili mbu na viuatilifu
tofauti ndani ya jamii moja kunaweza kupunguza shinikizo la uteuzi wa kiasili
linalochochea usugu wa viuatilifu.
“Kwa kuwakabili mbu na viuatilifu tofauti ndani ya
jamii moja, mbinu ya ‘micro-mosaic’ inaweza kupunguza shinikizo la uteuzi
linalochochea usugu, hivyo kufanya iwe vigumu kwa mbu kuzoea na kuwa sugu kwa
bidhaa moja tu,” walisema watafiti.
Hata hivyo, wameonya kuwa tafiti zaidi zinahitajika
ili kuthibitisha kama mkakati huo unaweza kupunguza usugu wa viuatilifu kwa
muda mrefu.
Iwapo tafiti zijazo zitathibitisha manufaa hayo, mfumo
wa “micro-mosaic” unaweza kusaidia kuhifadhi ufanisi wa viuatilifu vilivyopo
kwa sasa na kuongeza chaguo jingine muhimu kwa programu za kudhibiti malaria
katika kulinda jamii dhidi ya ugonjwa huo.
WANASAYANSI WA TANZANIA
Kavishe ni miongoni mwa wanasayansi wa Tanzania
walioshiriki utafiti huo, akiwa ni mwanabiolojia wa molekuli anayefanya kazi
katika tafiti za malaria ndani ya Idara ya Afya ya Mazingira na Sayansi za
Ikolojia katika IHI.
Amepata mafunzo ya kitaaluma katika biolojia ya
molekuli na amekuwa akijishughulisha na tafiti za malaria pamoja na magonjwa
mengine yanayoenezwa na wadudu kwa zaidi ya muongo mmoja.
Mbali ya Kavishe, mwanasayansi mwingine ni Dk. Samson
Kiware, mwenye Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi za Kompyuta za
Kihisabati (Computational Sciences).
Kwa sasa ni Mwanasayansi Mkuu wa Utafiti katika IHI,
ambako anaongoza Kitengo cha Takwimu za Juu na Uundaji wa Miundo ya Kihisabati
(Advanced Statistics & Mathematical Modelling Unit).
Aidha, ana nafasi za kitaaluma za heshima kama Profesa
Msaidizi wa Utafiti katika chuo kikuu cha Marquette na Profesa Mshiriki katika
Nelson Mandela African Institution of Science and Technology.
Hapo unapoishi, unaweza kushirikiana na majirani
zako kuwadhibiti mbu kwa mtindo huu?


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni