![]() |
| Vaileth Kimbe, akiwahudumia kuku wake: PICHA/Kijiji Chetu Media |
Huyo
ni Vaileth Kimbe (32), mfugaji na mjasiriamali ambaye sasa ameanza safari ya
kuwainua kiuchumi wasichana zaidi ya 3,000 kupitia mafunzo ya ufugaji wa kuku
na ujasiriamali.
Vaileth,
kupitia kampuni yake ya VIO FARM, anatarajia kuanzisha kituo maalumu cha
mafunzo kitakachowapa wasichana kutoka mazingira magumu maarifa ya ufugaji wa
kuku, elimu ya biashara na mtaji wa kuanzia wa Sh. 500,000 kila mmoja baada
ya kukamilisha mafunzo ya mwaka mmoja.
Anasema
dhamira hiyo imejengwa na uzoefu wake wa maisha pamoja na msaada alioupata
kutoka Shirika la CAMFED kupitia mtandao wa CAMA, ambao ulimwezesha kuendelea
na elimu wakati alipokuwa akikabiliwa na changamoto nyingi za kifamilia.
“Nilikulia
katika mazingira magumu na wakati mwingine niliona kama ndoto zangu hazingeweza
kutimia. Lakini nilijifunza kuwa changamoto si mwisho wa maisha, bali ni mwanzo
wa kupambana zaidi,” anasema Vaileth.
Akiwa
mwanafunzi wa kidato cha kwanza, alianza kuuza maandazi na bagia, ili kusaidia mahitaji ya
familia na kumsaidia mama yake. Juhudi hizo ziliendelea hadi alipopata ufadhili
wa CAMFED alipokuwa akisoma Shule ya Sekondari Luhota.
Kupitia
ufadhili huo alipata sare za shule, madaftari, vifaa vya kujifunzia na fedha za
matumizi, mahitaji muhimu yaliyomwezesha kuendelea na masomo bila
kukatisha ndoto zake.
Baada
ya kuhitimu elimu yake, Vaileth aliamua kuwekeza katika ufugaji wa kuku. Mwaka
2021 alipata mkopo wa Sh. milioni mbili kutoka CAMFED na
kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku wa mayai aina ya Sasso.
Leo
hii anafuga zaidi ya kuku 600 na huzalisha wastani wa trei 17 za mayai kwa
siku. Mafanikio hayo yaliongezeka mwaka 2025 baada ya kupata mkopo wa Sh. milioni 60 uliomwezesha
kujenga banda la kisasa lenye uwezo wa kuhifadhi kuku 3,000.
Kwa
Vaileth, mafanikio hayo si kwa ajili yake pekee. Anasema lengo lake kubwa ni
kuhakikisha wasichana wengine wanapata fursa aliyoipata ili waweze kujitegemea
na kufikia ndoto zao.
“Wasichana
wengi wana uwezo mkubwa. Wanachohitaji ni mtu wa kuwaamini, kuwapa maarifa na
mtaji wa kuanzia. Ninataka kuona wanasimama kwa miguu yao wenyewe na kubadili
maisha yao pamoja na familia zao,” anasema.
Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Iringa, Daudi Chilagane, anasema
ofisi yake imekuwa ikitoa ushauri wa kitaalamu kwa Vaileth ili kuhakikisha
anafanya ufugaji wenye tija na unaokidhi viwango vinavyohitajika.
Kwa
upande wake, mama yake Vaileth, Felister Nyalusi, anasema anajivunia mafanikio
ya mwanawe ambaye amepitia changamoto nyingi tangu akiwa mtoto.
“Alipambana
sana tangu akiwa mdogo. Leo hii si tu kwamba amebadilisha maisha yake, bali
ameanza kubadilisha maisha ya wengine. Hilo linanipa furaha kubwa,” anasema.
Katika
kipindi ambacho changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana inaendelea kuwa
miongoni mwa vikwazo vikubwa vya maendeleo nchini, juhudi za Vaileth zinatajwa
kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuwapa wasichana ujuzi wa vitendo, mtaji na fursa
za kujiajiri.
Kupitia
kituo chake cha mafunzo kinachotarajiwa kuanza kutoa huduma, maelfu ya
wasichana wanatarajiwa kupata maarifa yatakayowasaidia kujenga maisha bora na
kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao.
Kwa
Vaileth Kimbe, safari iliyoanza kwa kuuza maandazi na bagia sasa imekuwa mwanga
wa matumaini kwa kizazi kipya cha wasichana wanaotafuta njia ya kujikomboa kiuchumi.
![]() |
| Vailth Kimbe akiwa kwenye banda maalumu la kufugia kuku. PICHA: Kijiji Chetu Media |
KUHUSU CAMFED
CAMFED
(Campaign for Female Education), ni shirika la kimataifa lisilo la
kiserikali na lisilo la kibiashara lililoanzishwa mwaka 1993 kwa lengo la
kutokomeza umaskini barani Afrika kupitia elimu ya wasichana na uwezeshaji wa
wanawake vijana.
Shirika
hili linaamini kuwa elimu ni nyenzo muhimu ya kubadili maisha ya mtu mmoja
mmoja, familia na jamii kwa ujumla.
Tangu
kuanzishwa kwake, CAMFED imekuwa ikifanya kazi katika nchi mbalimbali za
Afrika, ikiwemo Tanzania, Ghana, Malawi, Zambia na Zimbabwe. Kupitia programu
zake, shirika hilo hutoa msaada wa kielimu kwa wasichana wanaotoka katika
familia zenye kipato cha chini ili waweze kuendelea na masomo bila vikwazo vya
kifedha.
Msaada
huo unajumuisha ada za shule, sare, vitabu, vifaa vya kujifunzia na mahitaji
mengine muhimu ya elimu.
Aidha,
CAMFED huendelea kuwasaidia wahitimu kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali,
uongozi, stadi za maisha na fursa za kupata mitaji kwa ajili ya kuanzisha au
kuendeleza biashara.
Moja
ya mafanikio makubwa ya CAMFED ni kuanzisha mtandao wa CAMA, unaowakutanisha
wanawake vijana waliowahi kufadhiliwa na shirika hilo.
Kupitia
mtandao huo, wanachama hupeana uzoefu, ushauri na kusaidiana katika miradi ya
maendeleo ya jamii; Vaileth akiwa mfano halisi wa matokeo ya
mtandao huu.
Tangu mwaka 2005, CAMFED imewafadhili wanafunzi 1,505,478 kuendelea na elimu ya msingi na sekondari katika shule 757 za serikali.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni