Jumamosi, 13 Aprili 2026 · Dar es Salaam, Tanzania
|
kijijichetumedia.com
Kijiji cha Habari Media
Kijiji cha Habari Media Simulizi za Mageuzi · SDGs · Tanzania
LEO
Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •    Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •   

Jumamosi, 16 Mei 2026

Courage House: Nyumba salama kwa mabinti walionusurika ukatili

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Courage House Dar es Salaam, Suzan Shoo, akisimulia jinsi nyumba hiyo salama inavyowapa matumaini mabinti walionusurika ukatili na usafirishaji haramu wa binadamu.

KUNA watoto ambao wamepitia mateso ambayo hata watu wazima hushindwa kuyasimulia bila kutoa machozi.

Wapo waliobakwa wakiwa na umri wa miaka 10. Wapo waliolazimishwa kujiuza ili familia ipate chakula. Wapo waliosafirishwa kutoka vijijini kupelekwa mijini kwa ahadi ya kazi nzuri, lakini wakajikuta kwenye mikono ya watu waliowageuza bidhaa.

Pamoja na maumivu hayo, kuna mahali panapoitwa Courage House — nyumba salama inayowarudishia watoto hawa utu na matumaini ya kufikia ndoto zao.

Katika ofisi ndogo yenye utulivu jijini Dar es Salaam, Suzan Shoo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Courage House Dar es Salaam, anasimulia kwa sauti ya utulivu, lakini yenye uzito wa maisha ya mamia ya mabinti waliopita mikononi mwao.

“Tunapokea mabinti waliopitia ukatili wa kingono na usafirishaji haramu wa binadamu. Wengine wanakuja wakiwa na majeraha ya mwili, lakini wengi zaidi wanakuwa na majeraha ya ndani kabisa,” anasema.

Safari ya Courage House ilianzia Marekani. Mwanzilishi wake, Jane Williamson, alikuwa na moyo wa kuwainua wanawake na kuwasaidia kufikia ndoto zao. Lakini maisha yake yalibadilika alipoona watoto waliokuwa wanaokolewa na serikali ya nchi hiyo baada ya kupitia ukatili wakikosa mahali pa kwenda.

Ndipo wazo la kuanzisha nyumba salama likazaliwa.

Kupitia marafiki waliokuwa wakifika Tanzania mara kwa mara, ndoto hiyo ilivuka mipaka na kufika Moshi, Kilimanjaro, ambako Courage House ilianzisha nyumba yake ya kwanza salama kwa mabinti waliookolewa kwenye mazingira ya ukatili.

Leo hii, Courage House inapokea wasichana walio chini ya miaka 18 kutoka maeneo mbalimbali nchini. Wengine wanaokotwa mitaani, wengine wanaokolewa kwenye nyumba za mateso, na wengine huletwa na maafisa ustawi wa jamii, polisi au asasi washirika.

“Mtoto akifika Courage anapewa kila kitu. Malazi, mavazi, chakula, matibabu, elimu, ushauri nasaha…tunaanza naye upya.”

“Tunapokea baadhi wakiwa na majeraha, wengine wamebakwa,” anasema Suzan kwa masikitiko.

Suzan anasema baadhi ya watoto wanaopokelewa wanakuja wakiwa na watoto au wakiwa wajawazito; huku wakiwa na maumivu makubwa moyoni. Anatoa mfano kwamba walimpokea mtoto aliyekuwa anabakwa na babu yake na mwingine amebakwa na baba yake hadi kupata ujauzito na kujifungua.

“Tunapompokea tunampa huduma zote hadi kujifungua na malezi yake na mtoto; kumsaidia kusoma yeye binafsi na mtoto.

“Kwenye kesi ambayo baba amehusika kumbaka binti ni ngumu sana kuitatua na kumwambia samehe…akimuangalia mtoto anasema huyu si ndugu yangu lakini ni mwanangu; tunafanya sana unasihi na maombi kwa sababu huyu anamaumivu makubwa moyoni,” anasimulia Suzan.

Anasema wengi wanakabiliwa na changamoto siyo ya elimu au chakula pekee, bali uponyaji wa ndani.

Anasema mbali ya ukatili wa kimwili na kihisia, asilimia 47 ya watoto wanaofikishwa Courage House huwa wamekatisha masomo katikati.

“Wengine wameishia darasa la sita, wengine kidato cha kwanza au cha pili, na baadhi hawajawahi hata kuingia shule.

“Tunawaanzisha shule upya. Kama alikuwa msingi tunamtafutia shule ya jirani. Kama hakuwahi kusoma kabisa tunamwingiza MEMKWA na wa sekondari tunampeleka QT. Lengo ni kuhakikisha mtoto anarudishiwa ndoto yake.”

Suzan anasimulia kuhusu mtoto mmoja mwenye miaka 10 waliompokea baada ya kujiingiza kwenye biashara ya ngono. Walipomhoji, alisema alianza baada ya kufanyiwa ukatili wa kingono nyumbani kwao.

“Alisema mama yake alikuwa anajua,” Suzan anasema kwa huzuni.

“Ukishakaa na mtoto kama huyu unamrudishaje kwenye familia ileile bila kubadilisha mazingira? Tunagundua kwamba wakati mwingine si mtoto tu anayehitaji kuponywa, hata mzazi anahitaji kubadilika.”

Kwa mujibu wa Courage House, asilimia 40 ya watoto wanaowapokea wana wazazi hai; tatizo ni kwamba wengi wao hawana ‘wazazi salama.’

“Wote hawana wazazi salama, hao wenye wazazi unakuta ndio waliochangia ukatili. Wazazi wengine wametengana halafu wenza wanaoona nao wanachangia kwenye ukatili…inategemea na matukio,” anasema.

Suzan anaongeza: “Wakati mwingine mtoto analazimika kwenda kujiuza ili familia ipate chakula. Hapo huwezi kutatua tatizo kwa kumrudisha tu nyumbani.”

Kutokana na hali hiyo, Suzan anasema Courage inatoa huduma za muda mrefu. Mtoto anaweza kubaki Nyumba Salama hadi afikishe miaka 18, akijengewa uwezo wa kujitegemea kabla ya kurudi kwenye jamii.

Anasema katika kipindi hicho, anakuwa ameelewa na kuona ubaya wa kurudi alikokuwa.

BAADA YA MIAKA 18

Mbali na nyumba ya watoto walio chini ya miaka 18, Courage House pia ina Transition House kwa waliovuka umri huo. Huko wanajifunza maisha ya kujitegemea — kuanzia elimu ya fedha, ujuzi wa kazi, hadi namna ya kuwa raia wema.

Wapo wanaosomea vyuo vikuu na wengine vyuo vya ufundi na hivyo wanaondoka Courage wakiwa wametimiza lengo la kupata elimu na ujuzi wa kuwawezesha kwenye maisha yao.

Suzan anatabasamu anaposimulia mafanikio ya mmoja wa mabinti hao.

“Tunaye msichana ambaye ndoto yake ilikuwa kuwa afisa ustawi wa jamii. Alikuja kwetu hajamaliza shule. Leo ameajiriwa Courage Moshi kama afisa ustawi. Mwingine yupo chuo kikuu anasoma Human Resources.”

Lakini hata baada ya watoto kuhitimu na kuondoka kwenye nyumba salama, Courage House hawaachi kuwafuatilia. Kupitia programu ya Baba na Mama Fellowship, vijana wanaomaliza masomo hupatiwa msaada wa kuanza maisha — godoro, gesi, vyombo na hata kodi ya miezi mitatu.

Siyo hivyo tu, Courage House inaendelea kuwafuatilia kwa upendo kuwapa malezi ya ziada (mentorship), ili wasimame kikamilifu na kufikia malengo makubwa ya maisha.

“Tunawauliza, kazi inaendeleaje? Unatunza fedha? Una mipango gani ya maisha?” anasema Suzan.

“Tunataka wajue kwamba bado wanapendwa.”

Suzan anasema lengo ni kuona mbegu waliyoipanda inazaa matunda ya mafanikio kwa watoto hao.

“Ni kumwambia kwamba umeshakuwa mtu mzima, kuwa raia mwema wa Tanzania ni hivi, mienendo hii ni sawa, tunatunza fedha namna hii, kipato chako ni hiki, tunza kiasi hiki. Je, unaenda kanisani au msikitini? Jenga imani.”

Kwa wale waliokuja na watoto au ujauzito wanapewa elimu ya malezi na makuzi ya mtoto.

Suzan anaeleza zaidi kwamba mwaka 2022 walifungua Courage Cafe Moshi Mjini— mgahawa unaouza kahawa na vyakula mbalimbali huku ukiwa sehemu ya kutoa elimu kuhusu madhara ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Anasema Courage inashirikiana na asasi nyingine za kijamii pamoja na serikali kutoa elimu hiyo.

“Dhana iliyopo ni kwamba watu wanafikiri usafirishaji haramu wa binadamu unatokea nje ya nchi, ambayo ni nusu ya ukweli. Unatokea hata ndani ya jamii yetu,” anafafanua.

Anasema ili kutoa elimu endelevu, imeanzishwa kampeni ya ‘Siyo ndani ya Nchi Yangu’ inyohimiza jamii kuepukana na usafirishaji haramu.

“Pale Courage Café kila anayenunua kikombe cha kahawa anachangia kuokoa maisha ya mtoto mmoja anayepitia ukatili,” anasema Suzan.

Leo, zaidi ya watoto 150 tayari wamepita Courage House na kuanza maisha mapya.

Anatoa wito kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao, kufuatilia mabadiliko ya tabia zao, na kujenga mazingira ya kuaminiana.

“Ukiona mtoto alikuwa mchangamfu ghafla anakuwa mkimya sana…wakati mwingine hiyo ni sauti ya maumivu,” anasema.

“Na mara nyingi wanaowaumiza watoto siyo watu wa mbali. Ni watu wa karibu kabisa.”

Anahimiza pia wazazi na walezi kuwa wabunifu kwenye shughuli za ujasiriamali, akisema hivi sasa kuna mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa na serikali kuwezesha biashara ndogo.

“Zipo shughuli nyingi sana za kujiingizia kipato halali na kutowaingiza watoto kwenye mateso ya ukatili. Wazazi waifuatilie waanzishe biashara ndogo kwenye mazingira yao,” anashauri Suzan.

MFAHAMU SUZAN

Ni mke na mama wa watoto wawili mwenye shahada ya Maendeleo ya Jamii na Uchumi.

“Nilianza Courage mwaka 2016 kule Moshi kama afisa ustawi wa muda nilikuwa nimeajiriwa sehemu nyingine. Nilifanya kwa muda…nipoanza kazi walikuwa watoto wanne.

“Baadaye nikaajiriwa full time…nikawa meneja wa Nyumba Salama Moshi, nikafanya kwa miezi kama nane hivi…ilipofika mwaka 2022 baada ya shirika kuona uhitaji Dar es Salaam nikahamishiwa hapa kama Ofisa Mtendaji Mkuu…tuna wafanyakazi 15 wa idara mbalimbali.

“Walimu, walinzi, wapishi, walezi na maofisa ustawi wa jamii. Tumeshahudumia takribani watoto 45 hapa Dar es Salaam tangu tulipoanza rasmi 2023. Ofisi ilianza mwaka 2022 lakini husuma ya Nyumba Salama ilianza mwaka uliofuata.

Suzan ni mwanamke anayethamini maisha ya wengine na ndio maana alikubali kufanyakazi na shirika dogo likiwa na watoto wanne pekee. Moyo wake wa kujitolea umeifanya safari yake ya miaka sita ndani ya Courage House kuwa ya mafanikio kutoka ofisa wa kawaida hadi Mtendaji Mkuu wa Taasisi. 

Umejifunza nini? Unataka kuchangia mabadiliko chanya kwenye jamii jamii, tuandikie maoni yako hapa nchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni