Jumamosi, 13 Aprili 2026 · Dar es Salaam, Tanzania
|
kijijichetumedia.com
Kijiji cha Habari Media
Kijiji cha Habari Media Simulizi za Mageuzi · SDGs · Tanzania
LEO
Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •    Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •   

Jumatatu, 11 Mei 2026

Star Homes zapunguza malaria kwa watoto Tanzania – Utafiti

 

Nyumba ya Star Homes mkoani Mtwara, iliyosaidia kupunguza malaria kwa watoto. PICHA: Ingvartsen Architects/Julien Lanoo.

Kuboresha mazingira ya makazi kunaweza kuwa silaha muhimu katika kupunguza magonjwa ya watoto nchini Tanzania, kulingana na matokeo ya utafiti mkubwa wa kisayansi uliofanyika vijijini na kubaini kuwa nyumba bora zina mchango mkubwa katika kulinda afya za watoto.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Nature Medicine Aprili 21,2026 ulifuatilia familia zilizoishi katika nyumba maalumu zinazoitwa “Star Homes” katika Mkoa wa Mtwara na kulinganisha afya zao na familia zilizoendelea kuishi katika nyumba za kawaida za vijijini kati ya mwaka 2022 na 2024.

Matokeo yake yanaonesha kuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano walioishi katika nyumba zilizoboreshwa walikuwa na viwango vya chini vya malaria, kuhara pamoja na maambukizi ya njia ya hewa katika kipindi chote cha miaka mitatu ya utafiti.

Utafiti huo umefanywa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali za kimataifa na Tanzania, zikiwamo Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), CSK Research Solutions, University of Oxford, Royal Danish Academy, Durham University, Amsterdam UMC pamoja na Mahidol-Oxford Tropical Medicine Research Unit.

Watafiti kutoka Ifakara waliohusika ni pamoja na Arnold Mmbando na Ally Olotu.

Katika utekelezaji wa mradi huo, nyumba 110 za ‘Star Homes’ zimejengwa katika vijiji 70 nchini mwaka 2021 na familia zilihamia kati ya Juni na Desemba mwaka huo.

Kuanzia Januari 2022, watoto 247 walioishi katika nyumba hizo walifuatiliwa pamoja na watoto 936 waliokuwa wanaishi katika nyumba za kawaida.

Ufuatiliaji wa afya ulifanywa kwa miaka mitatu kupitia ziara za kila wiki zilizofanywa na watafiti.

Matokeo yalionesha kwamba asilimia 98 ya watoto katika makundi yote mawili walikuwa wakitumia vyandarua, jambo lililowasaidia watafiti kubaini kuwa tofauti za kiafya zilichangiwa zaidi na mazingira ya makazi kuliko matumizi ya vyandarua pekee.

NYUMBA NI SEHEMU YA KINGA YA MAGONJWA

Matokeo hayo yanakuja wakati nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na changamoto zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi, usugu wa dawa na viuadudu vinavyotumika dhidi ya mbu, pamoja na mifumo ya afya yenye mzigo mkubwa wa wagonjwa.

Moja ya ujumbe mkubwa wa utafiti huo ni kwamba mapambano dhidi ya magonjwa hayawezi kutegemea hospitali na dawa pekee, bali yanahitaji pia mazingira bora ya makazi.

“Uboreshaji mkubwa wa usanifu wa nyumba za vijijini una uwezo wa kuleta athari kubwa ya kiafya katika maeneo ya Afrika yenye joto na unyevunyevu,” watafiti wamefafanua.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, asilimia 44 ya watoto walioishi ‘Star Homes’ walikuwa na maambukizi machache ya malaria, wakati magonjwa ya kuharisha yalipungua kwa asilimia 30 na ni asilimia 18 pekee waliokuwa na maambukizi ya njia ya hewa; ikilinganishwa na watoto walioishi katika nyumba za kawaida za vijijini.

Utafiti huo pia ulionesha maboresho katika ukuaji wa watoto pamoja na kupungua kwa tatizo la udumavu.

“Maambukizi ya magonjwa haya matatu makubwa yanayosababisha vifo vya watoto yanahusishwa kwa karibu na mazingira ya nyumbani,” wanaeleza watafiti.

UPEKEE WA STAR HOMES

Star Homes zilibuniwa mahsusi kupunguza hatari za maambukizi kupitia mifumo mbalimbali ya kisasa ya mazingira na afya.

Mwonekano wa nyumba bora za vijijini Mtwara/PICHA: Ingvartsen Architects/Julien Lanoo.

Sifa ya kipekee ya nyumba hizo ni kwamba zina madirisha yenye nyavu za kuzuia mbu, mfumo bora wa kuingiza na kutoa hewa, maeneo safi ya kupikia, mifumo ya kuvuna maji ya mvua, nishati ya jua, vyoo bora vya usafi wa mazingira na milango inayojifunga yenyewe kuzuia wadudu kuingia.

Nyumba hizo zinazojengwa kama ghorofa, vyumba vya kulala viliwekwa katika ghorofa ya juu, ili kupunguza uwezekano wa kung’atwa na mbu ambao mara nyingi huruka karibu na ardhi.

Zimetengenezwa kwa kutumia mbinu zinazotegemea mazingira ya asili bila matumizi makubwa ya nishati.

Watafiti wanasema nyumba nyingi za kawaida vijijini huwaweka watoto katika hatari kubwa kutokana na kung’atwa na mbu, kuvuta moshi wa ndani, hewa duni, uhifadhi usio salama wa maji na msongamano wa watu.

Kwa mujibu wa utafiti, changamoto hizo zinatatuliwa kwa wakati mmoja na ‘Star Homes’ na hivyo kutengeneza mazingira salama zaidi kwa watoto na familia zao.

“Nyumba bora zinaweza kupunguza mzigo wa magonjwa matatu hatari kwa watoto na kuboresha ukuaji wao,” watafiti wanafafanua.

STAR HOMES

Ni nyumba zilizobuniwa na kampuni ya Ingvartsen Architects chini ya uongozi wa Jakob Knudsen.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa awali wa kiuchumi, nyumba hizo; zinatumia saruji kwa kiwango cha chini kwa asilimia 73, zinapunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 57 na zilikuwa nafuu kwa asilimia 24 ukilinganishwa na nyumba za kawaida za saruji vijijini

Watafiti wanaamini matokeo hayo yanaweza kuwa muhimu kwa mustakabali wa Afrika, hasa wakati ambapo idadi ya watu barani humo inatarajiwa kuongezeka kutoka bilioni 1.5 hadi zaidi ya bilioni 3.7 ifikapo mwaka 2070.

Katika mazingira hayo, mahitaji ya mamilioni ya nyumba mpya yataongezeka, na tafiti kama hizi zinaonyesha kuwa nyumba hizo zinaweza kujengwa kwa njia ambayo si tu inalinda mazingira, bali pia inalinda afya za watoto.

MUUNDO WA UTAFITI NA WASHIRIKI

Ulikuwa ni utafiti wa majaribio uliokuwa wazi kwa washiriki na watafiti (open-label), uliotumia mfumo wa makundi ya kaya (household-cluster) pamoja na upangaji wa nasibu wenye udhibiti (randomized controlled trial), ambapo kila kijiji kilitumika kama kitalu cha utafiti. Utafiti huo ulifanyika kuanzia Januari 2022 hadi Desemba 2024.

Utafiti huo ulifanyika katika maeneo ya vijijini ya Mkoa wa Mtwara nchini Tanzania, karibu na mpaka wa Msumbuji.

Mkoa huo ulichaguliwa kwa kuwa ulikuwa miongoni mwa mikoa yenye kiwango kikubwa zaidi cha maambukizi ya malaria nchini mwaka 2023, ikiwa katika nafasi ya pili kitaifa. Aidha, kwa ujumla, asilimia 67.3 ya wakazi wa Mtwara walikuwa na upatikanaji wa vyandarua vyenye dawa ya kuua wadudu (ITNs).

Watafiti walifanya uchunguzi katika kaya 14,600 zilizopo katika vijiji 70 ambapo zilipatikana 862 zilizokuwa na sifa ya kushiriki.

Vigezo vilikuwa kukubali kushiriki katika utafiti kwa hiari, ikiwemo ufuatiliaji wa afya kwa kipindi cha miaka mitatu; kumiliki eneo la kutosha kujenga nyumba mpya; kaya kuwa na watoto watatu wenye umri chini ya miaka 13; na kuishi katika nyumba yenye kuta za udongo, paa la nyasi na sakafu ya udongo, ikiwa na choo cha shimo, bila umeme wala maji ya bomba.

Je, nyumba bora zinaweza kuwa silaha mpya ya kupambana na magonjwa ya watoto Tanzania?

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni