Jumamosi, 13 Aprili 2026 · Dar es Salaam, Tanzania
|
kijijichetumedia.com
Kijiji cha Habari Media
Kijiji cha Habari Media Simulizi za Mageuzi · SDGs · Tanzania
LEO
Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •    Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •   

Jumatatu, 4 Mei 2026

Safari ya mafanikio ya Bella Ragazza na mapambano ya vikapu asilia


PICHA: RESTUTA JAMES

Ule msemo wa anzia ulipo ukiwa na ndoto kubwa, umetafsiriwa kwa vitendo na nembo ya Bella Ragazza, iliyoasisiwa na mwanadada, Anna Ambroce, aliyeanza kutengeneza vikapu asilia akiwa na mwanamke mmoja mfumaji.

Safari ya Bella Ragazza ilianza mwaka 2018, lakini miaka saba baadaye, tayari alikuwa na wanawake 200 wanaofanyakazi hiyo na kujiingizia kipato cha uhakika.

“Tulianza tulikuwa na mama mmoja mwaka 2018, sasa hivi tuna wamama 200, ambao 100 wapo mkoa wa Iringa na 100 wapo Njombe,” anasema Shani ambaye ni meneja katika kampuni ya Bella Ragazza.

Aidha, anasema kazi hiyo imewezesha wanawake na vijana katika mikoa hiyo kujikwamua kiuchumi na kufungua biashara nyingine katika maeneo yao, baada ya kupata mitaji.

PICHA: RESTUTA  JAMES

“Wengi tofauti na maisha waliyokuwa wanaishi, maisha yameboreka. Wamejenga wengine wamefungulia biashara wanaume wao...kuna kijana ana miaka 21 amefungua saluni, amejenga, amenunua bodaboda na anamsaidia mama yake,” anaeleza.

Aidha, anasema pamoja na mafanikio hayo, wanakijiji hao wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa majani, kwani wafugaji wanayatumia kwa malisho na kisha huyachoma moto baada ya kuchunga ng’ombe.

“Changamoto kubwa ni majani mwanzoni walikuwa hawanunui, lakini sasa hivi wananunua...kule Iringa wafugaji wanaingiza sana ng'ombe porini halafu wakishalisha ng’ombe, wanachoma moto, kwa hiyo hawawaruhusu wale wamama kuchukua yale majani. Inawalazimu wale wamama waende Singida kununua,” anafafanua.

Shani anasema umbali wa kufuata majani unaongeza sio tu gharama ya usafiri bali pia usumbufu wa kulipa ushuru njiani.

“Wasipokuwa na kibali cha maliasili ni lazima ulipe ushuru, kwa hiyo inawawia vigumu sana kushona vikapu, sio kama ilivyokuwa mwanzo.

“Sasa hivi unaweza kuwaambia wakufumie vikapu 1,000 huwezi kupata vyote, utapata 500, kwetu ni changamoto kwa sababu unakuta kuna mtu wa jumla anavitaka. Je, utampa mtu wa jumla halafu dukani ukaacha usiweke. Inakuwa changamoto,” anasema Shani.

Anasema kikapu nacho kinalipiwa ushuru wa Sh. 500 hali ambayo inawakatisha tamaa baadhi ya wanawake ambao wangetamani kufuma vikapu katika muda wao wa ziada.

PICHA: RESTUTA JAMES

“Alipe ushuru, kibali, asomeshe watoto, alishe familia...hiyo hiyo hela ya vikapu. Ni changamoto.

“Ushauri wangu kwa serikali ni kwamba ipunguze ushuru na wale walioko kwenye halmashauri wangetembelea kwanza hivi vijiji. Mfano...Iringa wanaoshona vikapu wananyanyaswa sana na wafugaji...wanapeleka ng’ombe kula yale majani, wakimaliza kulisha wanachoma moto. Kwa hiyo hawa watu wa halmashauri wangewatembelea wajasiriamali wadogo kama hawa kujua changamoto zao...sio kukaa tu ofisini unaletewa makusanyo ya ushuru.

“Kwa kweli Halmashauri ndizo zinazotudidimiza,” anasema.

Anaongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, Bella Ragazza, imelazimika kukata kibali cha mwaka na kuwapatia wanawake wanaofanya nao kazi, ili kuwapunguzia usumbufu na kuwarahisishia kazi.

“Wamama hawana uwezo wa kulipa hizi gharama na zaidi sana watakata tamaa kwa hiyo sisi tuliamua kubeba hizi gharama,” anafafanua Shani.

MAFANIKIO

Pamoja na changamoto hizo, Bella Ragazza, inauza vikapu hivyo sio Tanzania pekee bali nje ya nchi hasa Ulaya na Marekani.

Bella Ragazza ni neno la Kiitaliano linalomaanisha “mwanamke mrembo,” lilichaguliwa na Anna baada ya kukaa kwa muda na Waitaliano na kuvutiwa na lafudhi yao.

Anna mzaliwa Iringa ambaye alibaini fursa ya soko la vikapu vya ambavyo alianza kwa kununua 53 kwa lengo la kuviongezea thamani.

Alianza na mtaji wa Sh. 500,000 akiwa peke yake, hivi sasa imeajiri watu kadhaa na kuwezesha wanawake na vijana 200 ambao wamepata soko la uhakika la vikapu, mikeka na viatu vya ngozi.

Nembo ya Bella Ragazza hutengeneza bidhaa zake kwa mikono, jambo linalofanya kila kipande kuwa cha kipekee na vya kuvutia sana.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni