![]() |
| Mpangilio wa vioo. PICHA: PINTEREST |
Ukiweza kutumia vyema vioo kuipamba nyumba yako, utabadilisha maeneo yote yanayoonekana kuwa ya kawaida kuwa ya kuvutia na yenye mwanga wa kutosha.
Vioo havifanyi kazi ya kuakisi tu; vinaweza pia kuinua
mtindo na mazingira ya nyumba yako.
Vinaweza kubadilisha chumba kwa namna zinazofurahisha
na zenye manufaa. Sio tu vinaakisi mwanga na kufanya nafasi ionekane kubwa na
angavu zaidi, bali pia ni kipengele muhimu cha usanifu kinachoipa nyumba yako
haiba ya kipekee.
Unaweza kuvitumia kuunda ukuta wa kumbukumbu wa vioo
(Gallery Wall), kwenye korido au sebule yako kwa kutengeneza ukuta wa kuvutia
wa maonesho ya vioo.
Mtindo huu wa mapambo unavutia kwa kuchanganya maumbo
na ukubwa tofauti wa vioo, na kuifanya nafasi yako ionekane kama onesho la
sanaa.
Hapa vitakusaidia kuongeza mvuto, mwanga wa asili na
kufanya hata kona ndogo na tulivu zionekane pana na za kuvutia.
Zingatia kuweka mkusanyiko wa vioo vya mviringo, mraba
na virefu vilivyowekwa fremu za mbao, chuma au hata rangi ang’avu vikipangwa
kwa ustadi ukutani.
DONDOO MUHIMU
Tatafuta vioo vyenye fremu za kipekee ili kuongeza upekee,
au tembelea maduka ya mitumba kupata vipande vya kipekee. Unaweza pia
kuchanganya picha za familia au michoro midogo ya sanaa ili kufanya ukuta huo
uwe wa kipekee, huku ukihakikisha mpangilio unabaki kuwa wa usawa na wenye kuvutia.
Tumia nafasi zinazofanana kati ya kioo na kioo ili
kuleta umoja wa muonekano. Ubunifu huu sio tu unapamba ukuta wako, pia unaakisi
lugha ya mtindo wako, na kuunda mazingira yenye ukarimu.
VIOO KWA WATOTO
Kwenye vyumba vya watoto, vioo vina nguvu kubwa sana
ya kuongeza msisimko; hivyo ubunifu utakamilisha hili. Kama watoto wanapenda
wanyama, masuala ya anga, mpira au kusoma, vioo hivi vinaweza kuwasha ubunifu
wao na kuwa kitovu cha kuvutia.
Unaweza kuweka kioo chenye umbo la nyota au mnyama
rafiki ili kubadilisha tendo la kawaida la kujiandaa kuwa tukio la kufurahisha.
Aidha, ili vioo hivi vya ubunifu vifanye kazi vizuri
katika chumba cha mtoto, fikiria mahali pa kuvipachika na matumizi yake. Tafuta
vioo vinavyoweza pia kuwa sehemu ya mwingiliano, ambapo watoto wanaweza kuchora
au kuandika ujumbe juu yake. Hii huongeza ubunifu wao na kufanya mapambo ya
chumba yao yawe ya kuvutia zaidi.
Tumia miundo inayohamasisha watoto kuchora au kuandika
na hakikisha rangi ya fremu inalingana na mandhari ya chumba.
UASILIA
Vioo vya mwonekano wa asili. Ikiwa unapenda joto na
haiba ya mapambo ya mtindo wa asilia, fremu ya vitu vya asili kama kinyago au
ukili, zinaweza kukamilisha mtindo wako. Mwonekano wake wa asili huleta hisia
ya ukarimu na urafiki katika chumba chochote.
Ili kufanikisha vyema, chagua fremu za mbao zilizotumika
(used), kwa mguso wa mazingira na pia tumia vioo vya mtindo wa zamani vilivyo
na muonekano uliochakaa kidogo.
Vichanganye na vitambaa laini ili kutengeneza mazingira
ya uasilia.
Vipachike karibu na vyanzo vya mwanga wa asili ili
kuongeza mwangaza.
Aidha, unapochagua kioo, ukubwa ni jambo la msingi.
Fikiria mahali unapotaka kukiweka. Kioo kikubwa kinaweza kuunda hisia ya nafasi
kubwa zaidi katika chumba kidogo. Pima eneo la ukuta ili kupata wazo la ukubwa
unaofaa. Kwa mfano, kioo kinapaswa kufunika angalau theluthi mbili ya nafasi ya
ukuta juu ya sofa au meza ya pembeni, ili kuleta mwonekano uliosawia.
Angalia mapambo yaliyopo tayari nyumbani kwako na uchague
vioo vinavyokamilisha samani na mapambo yako. Kwa mfano, kioo cha mtindo wa
zamani kinaweza kuongeza ladha ya jadi, huku kioo chenye muundo wa kisasa
kikaongeza mwonekano wa aina hiyo. Maumbo pia ni muhimu; vioo vya mviringo hunogesha
zaidi mwonekano wa chumba, wakati vile vya pembe nne huongeza mguso wa kisasa.
FREMU
Fremu ya kioo ina athari kubwa katika mwonekano wake
wa jumla. Fremu za mbao huleta joto na muundo wa asili, huku fremu za chuma
zikitoa mwonekano safi na wa kisasa.
Jambo la kuzingatia ni namna unavyotaka kutumia kioo
chako. Kioo kwa ajili ya kupaka vipodozi kinachopachikwa ukutani kinaweza kuwa
na sehemu ya kukuza taswira, wakati kioo cha mapambo kinaweza kuwa kwa
madhumuni ya kupendezesha tu.
Unapofikiria kuweka kioo, usisahau kufikiria kuhusu
mwanga! Vioo vinaweza kuakisi mwanga na kufanya maeneo yenye giza yaonekane
angavu zaidi. Weka vioo mkabala na madirisha au vyanzo vya mwanga ili kupata
matokeo haya.
Fikiria mkusanyiko wa vioo uliopangwa kwa ustadi, kila
kimoja kikirejesha mwanga na kuboresha mazingira ya chumba.
Kwa mpangilio mzuri wa vioo, changanya vioo vya
mviringo na vya mraba ili kuongeza mvuto. Pia unaweza kuongeza vipengele
vingine vya mapambo kama sanaa ya ukutani ili kuweka muonekano uliokamilika.
Mbinu hii bunifu hufanya nafasi yako kuwa ya kipekee
na kuruhusu mtindo wako binafsi kuonekana wazi.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni