![]() |
| Christowelu akiandaa vifaranga |
Habari mbaya za
kutofanikiwa kwa kilimo cha matikiti miaka ya 2014 pamoja na ufugaji wa samaki
kutofanya vizuri sokoni, hazikufanikiwa kuua ndoto ya Dk. Christowelu Zephania.
Badala yake, habari
hizo zilimfanya atafakari kwa kina kile alichopenda kukifanya kutimiza lengo
lake la kuipa jamii suluhisho la uhakika katika ufugaji; ndipo wazo la Fuga
Kuku Business Solution, likazaliwa na kuanza kuchanua rasmi.
Christowelu, Mkurugenzi
na Mwanzilishi wa kampuni ya Fugakuku Business Solution, ambaye kitaaluma ni
daktari wa mifugo, amefanikiwa kubadilisha ndoto za wafugaji zaidi ya 2,000
kuwa miradi ya kibiashara.
Anasema alipohitimu
chuo cha mifugo Buhari kilichopo mkoani Tanga, alipata ajira ambayo aliitumikia
kwa wiki moja pekee na kuamua kujiajiri kwa lengo la kuwa miongoni mwa watu
wanaoleta masuluhisho kwenye changamoto zinazoikabili jamii.
Anasema alilazimika
kufanya hivyo akiuza utaalamu wake kwa kuwafundisha wafugaji wapya ambao
hawajui chochote kuhusu ufugaji wa kuku, mbinu za ufugaji wa kibiashara, aina
za kuku, dawa, chakula, usafi na uzingatiaji wa chanjo.
Mwanadada
Christowelu, anasema kuku wanaofaa kufugwa kibiashara ni wa nyama, mayai na
chotora; akishauri kwamba kwa mfugaji mdogo anashauri aanze kufuga kuku wa
nyama ambao wanaweza kurudisha uwekezaji na faida baada ya siku 28.
Anasema safari yake
ya ujasiriamali ilianza mwaka 2014, kwa kushirikiana na mume wake, walikuwa
wanafanya miradi mitatu ya ufugaji wa kuku, samaki na kilimo cha matikiti;
miradi ambayo haikuwapa matokeo waliyoyakusudia.
Anasema wakulima wao
walishindwa kushindana sokoni hususani wa samaki ambao mazao yao hayakuwa na
samaki wakubwa kama ilivyotarajiwa.
“Tulifanya samaki,
watu hawakupata matokeo mazuri, kwa sababu samaki kwenye soko liliwashinda…mtu
anategemea kupata samaki wakubwa, anapata wadogo wadogo kwa hiyo mfugaji
anaingiza pesa lakini hapati faida…na kwenye matikiti vile vile…ndipo
tukafikiria tufanyeje…tukajikita kwenye ufugaji kuku.
“Mwaka 2016…ndio
tukajikita sasa, tukaangalia ni kitu gani ambacho mfugaji yeyote anaweza
kufanya kwa urahisi na kikamletea matokeo. Tukaamua kubaki na mradi mmoja wa kuku
peke yake.
“Tunawafundisha namna
ya kulea vifaranga, makundi ya chakula, dawa na kubwa zaidi usafi wa vyombo vya
chakula…aina zote tatu za kuku zinamakundi tofauti ya vyakula.
“Kwenye ufugaji wa
kuku kuna changamoto mbili…mtaji na magonjwa ya kuku. Watu wengi wanaanzisha
miradi ya kuku wanaishia katikati kwa sababu ya kuingiliwa na magonjwa. Namna
ya kukabili magonjwa ni kwa kuzingatia chanjo, lakini kubwa ni bio security
(usafi), kuzingatia usafi kwenye mabanda, vyombo vya chakula na mazingira yote
kwa ujumla,” anasema.
![]() |
| Christowelu akiwa kwenye moja ya mradi wa kuku |
Christowelu anasema kwenye
ufugaji wa kuku kibiashara, wameona matokeo makubwa na wateja wao wanapata
matokeo waliyoyakusudia.
“Kwa hiki
ninachofanya, naona wafugaji wakifanikiwa…kuku ni pesa, kuku ni biashara rahisi
kukua,” anasema.
Christowelu anasema
Fugakuku ni biashara ya familia, akishirikiana na mume wake ambaye ni mtaalamu
wa majengo (architecture).
“Kwenye ujenzi wa
mabanda yeye ndilo eneo lake hasa. Tukija kwenye menejimenti na ufugaji
kibiashara mimi ndio naingia. Yeye pia anajua kila kitu kuhusu kuku,” anasema.
Christowelu ambaye
ametoa mafunzo kwa zaidi ya wafugaji 2,000, anasema changamoto anayoiona kwa
jamii ni kutokuwa na taarifa kuhusu ufugaji.
“Watu wengi bado
hawana taarifa za kuku…tumefanya hii kazi kwa miaka 10 sasa, watu wanamchukulia
kuku kama ni ndege mdogo, ambaye hana thamani. Unaweza ukamtembelea mfugaji
akadhani kujenga banda la kuku 2,000 ni Sh. 300,000…changamoto nyingine ni
mitaji. Ili uweze kufanya kwa ukubwa lazima uwekeze kikubwa. Kuku huwezi
kufanya kwa Sh. 100,000,” anafafanua.
Kuhusu mtaji alioanza
nao yeye, Christowelu anasema walikopeshwa kiasi cha fedha na wazazi wa mume
wake, ambacho walitumia kununua vifaranga na kulipa fedha kidogo kwa ajili ya
mashine ya kutotolesha vifaranga.
“Lakini pia tulikuwa
tunauza utaalamu kwa maana ya kufundisha watu, tunatembelea mashamba ya
wafugaji na tuliendelea kutumia mitandao ya kijamii kujitangaza.
“Tumehudumia zaidi ya
watu 2,000…tumeanyakazi Dodoma, Morogoro, Geita, Arusha, Mbeya, Tanga na Mtwara
na hapa Dar es Salaam ambako ndipo zilipo ofisi zetu. Mikoa mingine tumeuza
ujuzi, vifaa na vifaranga.
Kwenye ujuzi anasema
Fugakuku Business Solution, inatoa elimu kuhusu ufugaji wa kuku, makundi ya
chakula, muda wa kuwalisha, utoaji wa chanjo na usafi wa mabanda na vyombo vya
chakula.
Anasema wanauza pia vifaranga,
wanajenga mabanda na wanasambaza vifaa vya kuku kama incubator.
“Kuku ni pesa
inayotembea…ninatoa rai kwamba watu waanzishe mradi wa kuku. Anza tu ukiwa
mdogo, chini kabisa anza na kuku 200. Unaweza kuongeza kuku hadi mara tatu kwa
mwaka. Ni mradi ambao unakufanya uendelee na shughuli zako kama kawaida,
zingatia usafi na chanjo,” anasema.
Kuhusu matumizi ya mitandao anasema ndiyo iliyobadilisha maisha yao kwa kuwa ni jukwaa linalowapatia wateja ndani na nje ya Dar es Salaam.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni