Jumamosi, 13 Aprili 2026 · Dar es Salaam, Tanzania
|
kijijichetumedia.com
Kijiji cha Habari Media
Kijiji cha Habari Media Simulizi za Mageuzi · SDGs · Tanzania
LEO
Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •    Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •   

Jumatatu, 13 Aprili 2026

Wise Pill Box: Teknolojia mpya ya kufuatilia dawa za TB na kupunguza usugu

 

Wise Pill Box

TEKNOLOJIA ya Wise Pill Box inaleta mapinduzi katika ufuatiliaji wa matumizi ya dawa za kifua kikuu (TB), kwa kusaidia wahudumu wa afya kufuatilia wagonjwa kwa wakati halisi.

Kwa kifaa kidogo kinachobebwa mkononi, wahudumu wa afya wanaweza kujua kwa wakati halisi kama mgonjwa amemeza dawa—au ameacha.

Ubunifu huu wa kidijitali kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), unalenga kupunguza usugu wa dawa na kuboresha matokeo ya matibabu.

Kwa lugha rahisi ni kwamba Wise Pill Box ni kisanduku janja cha dawa kinachozungumza na hospitali.

Kila mgonjwa anapokifungua kuchukua dawa taarifa hutumwa moja kwa moja hospitalini, mfumo huandika muda halisi wa matumizi ya dawa na kama hakijafunguliwa, tahadhari hutumwa.

Mtafiti Mkuu wa miradi ya TB katika Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk. Beno Mbeya, anasema kifaa hicho kinamsaidia mtoa huduma za afya kufuatilia wagonjwa wake wa TB kwa urahisi na kutoa ushauri kwa wakati.

Anasema kifaa hicho kinampa taarifa mtoa huduma wa afya aliye hospitali pale mgonjwa anapomeza dawa au asipomeza; kikirekodi muda aliomeza.

Wise Pill Box

“Ni kifaa kinachochajiwa na kinakaa na chaji kwa miezi mitatu…mgonjwa akikifungua kinatoa taarifa hospitali kwenye simu au kompyuta. Mgonjwa asipomeza dawa pia kinatoa taarifa. Inakuwa rahisi mtoa huduma kumfuatilia mgonjwa na wakati mwingine unaweza kumpigia simu kumkubusha kumeza dawa,” anasema.

Anakumbusha kwamba matibabu ya TB kwa kawaida huwa ni ya muda mrefu; ikiwa ni miezi sita kwa wagonjwa wa kawaida na inafika miezi tisa mpaka 24 kwa wale ambao wana kifua kikuu sugu.

“Kutumia dawa za kifua kikuu huwa zinakuwa nyingi, unaweza kupewa dawa tofauti tofauti nne, na unameza kwa miezi sita kila siku bila kusimama. Usipomeza kama inavyotakiwa unatengeneza usugu, unaweza usipone, unaweza ukasambaza wadudu zaidi…na tunajua kuna athari za hizi dawa za TB, kwa hiyo ili kuhakikisha mgonjwa anameza hizi dawa, kwa wakati, kila siku bila kupoteza dozi, tunatumia digital technology, kuhakikisha kwamba kweli mgonjwa anameza dawa.

“Tunaweka dawa kwenye wise pill box, anaenda nacho nyumbani, ule muda wa kunywa dawa ukifika, akikifungua, sisi tunapata ujumbe.

“Inatuambia mgonjwa amemeza dawa saa ngapi na kama hajafungua, tunajua mgonjwa huyu hajameza dawa; hii ndio device ambayo tunaitumia.

“Tumeanza kukitumia mwaka juzi (2024), lakini bado kipo kwenye majaribio, ila kinaleta matokeo yenye matumaini.

“Utafiti huu kwa sasa tunaufanyia Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, sisi Ifakara tuna kituo chetu cha utafiti ambacho tunafanya tafiti za kifua kikuu.

Huu mradi una awamu tofauti tofauti, awamu ya kwanza ilikuwa na wagonjwa 28 na hao walipewa hii device,” anafafanua Dk. Mbeya.

Naye Mfamasia Mtafiti wa dawa na chanjo katika taasisi hiyo, Beatus Simon, anasema mgonjwa anapokuwa amemeza dawa, taarifa inayopokelewa inaonesha muda na kuweka alama ya bluu wakati kwa wale wasiomeza dawa inatuma taarifa ya kijivu.

Anasema mgonjwa wa TB anapaswa kuzingatia umezaji wa dawa katika muda unaofanana kila siku, ili kuhakikisha vimelea havipati usugu wa dawa.

Wakati wakibaini kifaa hicho, takwimu zinaonesha kwamba Mkoa wa Dar es Salaam (Temeke), unaongoza kwa ugonjwa wa TB; ikifuatiwa na Kilimanjaro, Dodoma, Mbeya na Mwanza.

Aidha, Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye mzigo mkubwa wa TB unaotajwa kuwa miongoni mwa magonjwa hatari zaidi ya kuambukiza duniani licha ya uwepo wa matibabu.

Hata hivyo, hapa nchini visa vipya vimepungua kwa asilimia 44, kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi 172 kwa kila watu 100,000 mwaka 2024.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya Mwaka 2024, inaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Aidha, vifo vitokanavyo na ugonjwa vimepungua kutoka 56,000 mwaka 2015 hadi vifo 23,500 mwaka 2024, sawa na punguzo la asilimia 59. Kiwango hiki kimepelekea Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache duniani zilizo katika hatua nzuri ya kufikia lengo la dunia la kutokomeza ugonjwa huu ifikapo 2030.

MWANASAYANSI NYUMA YA UVUMBUZI

Dk. Beno Mbeya

Nyuma ya mafanikio haya yupo Dk. Beno Mbeya, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya mapafu, akiwa ameongoza tafiti kadhaa za TB (Optirimox, STEP 2C, DECODE TB).

Ana utaalamu katika afya ya umma na teknolojia za afya, kazi yake inaunganisha sayansi, teknolojia na maisha halisi ya wagonjwa.

Mwanasayansi huyo ambaye ni mtafiti katika Taasisi ya Ifakara (IHI), tangu mwaka 2013.

Ana msingi imara wa kitaaluma na uzoefu mpana wa kitaalamu katika nyanja ya afya ya umma. Ana shahada ya Udaktari wa Tiba (Doctor of Medicine) kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Afya ya Umma (MSc Public Health), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kabla ya hapo, alipata pia Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA) kutoka chuo hicho.

Dk. Beno kwa sasa anasoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Afya ya Umma katika Chuo Kikuu cha Nicaragua (Hispania), ambapo anatarajiwa kuhitimu mwaka huu 2026.

Mbali na hilo, Beno anatoa huduma zake kama Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mapafu (Consultant Pulmonologist); anashirikiana na taasisi na mashirika mashuhuri kama Medical Association of Tanzania, mtandao wa TB Net consortium, pamoja na vikundi mbalimbali kama Trial Methodology Research Partnership (TMRP)/NIHR nchini Uingereza. Mchango wake unahusisha maeneo mbalimbali ikiwemo tathmini ya matokeo ya tiba, mifumo ya taarifa za afya (health informatics), na tiba inayolengwa kulingana na sifa za mgonjwa (stratified medicine).

Unadhani teknolojia kama hii inaweza kusaidia wagonjwa katika jamii yako?

Tuandikie maoni yako na sambaza makala hii ili kuongeza uelewa kwa watu wengi zaidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni