UBORA wa meza za konsoli (console table), unatokana na
ubunifu wa kuipamba kwa vitu vya kuvutia macho. Ni muhimu vitu vinavyopamba
meza hii viwe vichache lakini vinavyovutia macho na visivyochosha akili wala
kukinaisha ubongo.
Ni sehemu unayoweza kuweka mimea ya kijani kama maua
ya ndani, kioo, taa, mshumaa, picha, vitabu au pambo asilia.
Pia unaweza kuifanya meza hii kuwa na mguso binafsi
kwa kuweka pambo la msimu ili kuongeza haiba, huku ukizingatia uwiano wa vitu
virefu na vifupi, kuiongezea mvuto wa kuonekana.
Mawanda ya kuipamba meza hii ni mapana kinachotakiwa
ni mbinu sahihi na uhalisisa wa tukio lenyewe ikiwa utaipamba kwa shughuli
mahsusi kama ‘siku ya wapendanao.’
Unaweza kujumuisha mimea inayoongeza hewa ya oksijeni
kama ulimi wa mamamkwe, ua pesa, ZZ, na mengineyo; ili kuongeza mzunguko mzuri
wa hewa ndani. Hapa inashauriwa utumie majagi ya kioo kuleta rangi ang’avu na
kuongeza hali ya uhai.
Unaweza pia kuweka kioo kikubwa (cha duara au
mstatili), ambacho ukikiweka kimkakati kinaongeza nafasi na kuruhusu mwanga
kuenea.
Pia unaweza kutumia vitabu kubadilisha meza ya konsoli
kutoka kuwa ya kawaida na kuifanya kuwa kitovu cha macho. Uchaguzi makini wa
vitabu huongeza mvuto wa kuona, hasa unapojumuisha jalada zenye rangi ang’avu
zinazoendana na mpangilio wa rangi wa mapambo.
Kupanga vitabu kwa mlalo na kwa wima huongeza urefu na
muundo, huku pembe tofauti zikilainisha mpangilio.
Sanaa ina uwezo wa kipekee wa kubadilisha meza ya
konsoli na kuifanya kuwa ya kipekee kama utafanya uchaguzi makini wa michoro au
picha za sanaa, zenye upana wa takribani theluthi mbili hadi robo tatu ya upana
wa meza.
Unaweza kuongeza matumizi bila kuathiri mtindo, kwa kujumuisha viti vya umbo la mchemraba, hivyo kuongeza mapambo yenye matumizi huku nafasi ikibaki nadhifu.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni