WATU wengi wanakwama kuanzisha bustani ya maua nyumbani
kwa kufikiria gharama kubwa za nyasi, maua, vyungu, mbolea na udongo.
Wanasahau kwamba ubunifu wa kupangilia vyema maua yanayoonekana
kuwa ya kawaida, ni njia bora kabisa ya kuwa na bustani yenye mvuto na utulivu
nyumbani.
Mathalani, bougainvillea ni ua linalostawi katika
mazingira mengi, likistahimili hali ya hewa mwaka mzima; likitajwa kama kitovu
cha mandhari tulivu ya nje.
Likitunzwa vizuri, maua yake yenye rangi ang’avu,
mchanganyiko wa nyeupe na waridi, huunda kivutio kikuu dhidi ya mandhari nyumbani,
meupe yakisanifisha usafi na kuongeza hisia za furaha na mahaba.
Likiwa chini ya mti linamsaidia mtu kupata sehemu yenye kivuli cha kupumzika na kutafakari, huku likichochea mandhari asilia inayochochea utulivu wa mwili na akili.
Sifa kuu za bougainvillea ni rangi zake ang’avu,
urahisi wa kulitunza na ukuaji wa haraka. Ukilitunza kwa usahihi, bougainvillea
inaweza kukua vizuri katika maeneo mengi, likiwa na rangi ya waridi, zambarau,
chungwa na nyeupe.
Linapenda hali ya hewa ya joto (juani), udongo unaopitisha
maji vizuri ili kuzuia mizizi kuoza; na katika mazingira haya, utalifurahia kwa
kuchanua kwake mwaka mzima.
Ili kulihakikishia uhai, hakikisha eneo ulipolipanda
hakutwami maji. Unaweza kuongeza changarawe au vipande vya vyungu
vilivyovunjika kwenye shimo la kupandia.
Aidha, ukiona majani yaliyonyauka au kuwa ya njano tambua
kuwa ni dalili ya ukosefu wa maji na ukiona majani yakilegea au kudondoka,
huashiria umemwagilia maji mengi kupita kiasi.
Pamoja na kwamba bougainvillea linaweza kustahimili
ukame kwa kiasi, lakini bado linahitaji maji. Lipatie maji ya kutosha, lakini ili
kuimarisha mizizi si mara kwa mara.
Unapolipogoa unaimarisha afya yake, wataalamu wa
bustani wakisema kwamba kulipogoa mara kwa mara kunawezesha kutengeneza umbo
ulipendalo na kuchochea ukuaji mpya.
Wataalamu wanapendekeza upogoaji ufanyike wakati wa masika
baada ya baridi kuisha kwa kuondoa matawi yaliyokufa au kuharibika na kupunguza
matawi marefu, ili kudhibiti umbo na ukubwa.
Inashauriwa kulisaidia katika kutengeneza umbo au
kulielekeza kupanda kwenye mti au ukuta, ili kufurahia uzuri wake.
Kwa matunzo sahihi, unaweza kukuza bougainvillea yenye
maua ya kuvutia sana. Unahitaji kuchagua eneo sahihi, kupogoa, kumwagilia na
kutia mbolea. Dondoo hizi zitakusaidia kukuza bougainvillea yako kwa mtindo uupendao.
DONDOO MUHIMU
Unaweza kulipanda kwenye poti lenye ukubwa wa lita 30
na ukazipanda aina tatu kwa pamoja.
Likikaa juani na likatunzwa vizuri linachanua mwaka
mzima.
Ni mmea wa kupanda (climber), hivyo unahitaji uusaidie
kupanda unavyotaka, ikiwa ni ukutani au kwenye mti.
Halihitaji maji mengi, linafaa maeneo yenye mvua
chache.
Linahitaji mbolea ya wastani na hivyo kulifanya kuwa
mmea usiohitaji gharama kubwa.
Kwa ufupi, bougainvillea ni chaguo bora kwa yeyote
anayetamani bustani ya kuvutia, tulivu na rafiki kwa mazingira bila kuumiza
mfuko. Ni ushahidi kuwa uzuri wa asili unaweza kupatikana kwa ubunifu mdogo na
matunzo sahihi.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni