MUHTASARI
Misheck Lwenje ni kijana wa Kitanzania aliyethibitisha kuwa kilimo ni ajira na biashara yenye tija. Kutoka kujitolea bila malipo hadi kujiajiri, Lwenje amewezesha zaidi ya wakulima 2,000 kupitia mbinu za kilimo biashara na umwagiliaji rahisi. Safari yake ilianza na mtaji wa Sh. 600,000 uliozaa shamba lenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 40, na leo anaongoza Kilimohalisi kama jukwaa la mafunzo, ajira na matumaini mapya kwa vijana na wakulima.
Ukiona posti zake kwenye mitandao ya kijamii akiwa ‘mchafumchafu’, huwezi kudhania kwamba Misheck Lwenje, ni kijana mwenye akili nyingi, ambaye amewafundisha wakulima zaidi ya 2,000 mbinu za kilimo biashara kwa umwagiliaji rahisi.
Lwenje mhitimu wa Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA) mwaka 2015, ambaye
yuko nyuma ya Kilimohalisi, hakuhitimu na kuanza kufundisha wakulima, bali
kujitolea kwake, uvumilivu na nidhamu ya matumizi ya kila shilingi anayoipata,
vimemfikisha alipo sasa.
Akiwa na Sh. 600,000 aliamua kununua shamba ambalo
kimsingi ndio ofisi yake inayomwingizia kipato; na tayari limeongezeka thamani
hadi zaidi ya Sh. milioni 40, ndani ya miaka minne.
Anafundisha matumizi ya kila kipande cha ardhi kwa
kilimo cha biashara, kilimo bila kemikali, mbinu rahisi za umwagiliaji na umuhimu
wa kupanda mimea ya kudhibiti wadudu waharibifu.
“Nilipomaliza
haikuwa rahisi kupata ajira; kwa hiyo nikawa nimeomba kujitolea kampuni moja
iko Iringa inayohudumia wananchi. Nikafanya kazi kama miezi sita nikawa
silipwi, lakini nikawa napata maarifa na ‘connection.’
Anasema
kujitolea kwake hakukuwa bure kwani miezi sita baadaye alikutana na watu wengi
pamoja na taasisi mbalimbali, akiwamo mwajiri wake wa kwanza, kampuni ya
kimataifa inayojishughulisha na kilimo kutoka Kenya.
Anasema
mwishoni mwa mwaka 2016, kampuni hiyo ilisitisha kazi nchini na kulazimika
kurejea Dar es Salaam kuendelea kujitafuta.
“Nikiwa
nyumbani Dar es Salaam, alikuja rafiki yangu kwenye usaili, akashukia kwetu na
ikalazimu asubuhi nimsindikize, tulipofika kwenye lile shirika (la Norway),
jamaa aliyetupokea akasema basi ingieni wote (kwenye
usaili)…maswali
waliyouliza mimi nilikuwa nina uzoefu nayo kwa hiyo nikajibu vizuri sana,
akasema atatuchukua wote kwa hiyo nikapata kazi.
“Tulikuwa
tunawafundisha watoto yatima namna ya kujiajiri kupitia kilimo
na tulikuwa
tunafanya hivyo kuwaandaa kujitegemea.
“Baadaye
wakaniambia niwafundishe wanawake kwenye Vikoba, kukawa na mkutano wa vikundi
vya vikoba kutoka mikoa mbalimbali Tanzania. Hapa nikaendelea kuongeza maarifa
na kujifunza zaidi,” anasema.
Lwenje anasema baada ya mkutano wa VIKOBA, viongozi
waliomba mafunzo kwenye mikoa yao na ndipo yeye akapangiwa kwenda kufundisha
wilayani Chunya, mkoa wa Mbeya.
“Tulikuwa
tunawafundisha kufunga mfumo rahisi wa umwagiliaji…nilifanyakazi Mbeya, Songwe,
Manyara na kisha Hai-Kilimanjaro hadi mwaka 2021 mkataba ulipoisha nikakataa
kuendelea kuajiriwa,” anasema Lwenje.
Lwenje
ambaye amejikita kwenye kilimo cha mboga, anasema kazi hiyo alianza kuifanya
kwa kuzalisha miche na kuwafungia wakulima mfumo rahisi wa umwagiliaji.
“Unaona
hii kazi ninayoifanya nilianza kuifanya bure, nilikuwa nazalisha miche, nawapa
watu bure. Hata mfumo wa umwagiliaji nilikuwa nawapa watu bure. Nilitafuta site
ambazo watu wengi wakipita wanaweza kuona…mtu akitaka kufanya kitu namwambia
nenda kaangalie sehemu fulani, ukipenda uje tufanye kazi; nilianza kufanya bure,
nikaanza kupata pesa baada ya watu kupenda.
“Nilitengeneza
wakulima wa mfano na baadaye nikaanza kupata fedha. Nilianza kazi hii nikiwa na
vijana wawili, lakini hivi sasa nina timu ya watu zaidi ya 20 ambao ninafanya
nao,” anafafanua.
Mbali ya kufundisha wakulima, Lwenje anasema Kilimohalisi
ni kiwanda cha kupika wataalamu wa kubobea kwenye kazi, wanaoweza kuajiriwa na
kampuni yoyote.
“Mafanikio
makubwa niliyopata ni kutengeneza watu ambao wanaweza kuajiriwa na watu wengine
kutokana na kwamba wana uzoefu,” anafafanua.
FURSA KWENYE KILIMO
Anasema
watu wanapaswa kufahamu kuwa mabadiliko ya tabia nchi yamepunguza uzalishaji wa
chakula duniani, ilihali kuna ongezeko kubwa la watu wanaohitaji chakula kila
siku.
“Nawaambia
vijana kwamba kilimo ni fursa, hata kama atachelewa kuiona hela, lakini
ataipata; cha kwanza kwenye kilimo kila mtu anahitaji chakula.
“Chakula
ni sehemu nyeti sana duniani, ukiangalia hata magonjwa mengi tunayoyapata
yasiyoambukiza asilimia kubwa yanasababishwa na chakula, tunakula vyakula
ambavyo hatujui vimetoka wapi na amepiga dawa lini, hii ni changamoto kubwa.
“Fursa
kwetu ni kubwa sana kwa sababu tunaweza kuzalisha chakula salama na tukaenda
kuuza nje…hii ni fursa kwa vijana na kwenye soko la ndani fursa ni kubwa sana,”
anafafanua Lwenje.
Anasema
ili kufanikiwa kwenye kilimo, ni muhimu kuzalisha chakula kizuri kisicho na
kemikali kwa kuzingatia muda wa kupiga dawa na kuvuna, ili kuwahakikishia
walaji usalama wa afya.
Hata
hivyo, anashauri ni muhimu kuwa na bustani ya mboga nyumbani ili kila familia
ijipatie chakula salama.
ALIKOANZIA
Anasema
safari ya Kilimohalisi ilianza mwaka 2019 alipopata Sh. 600,000 akanunua
shamba ambalo limekuwa ofisi yake.
“Ni
juzi tu kuna mtu amenifuata anataka kulinunua kwa Sh. milioni 40
nikakataa…lakini kama mwaka 2019 ningeamua kununua simu mpya nzuri au
gari, nisingekuwa nayo na wala nisingekuwa na shamba. Ninachotaka kusema ni
kwamba vijana tuwe na vipaumbele na sio kufanya vitu kwa kujionesha au kufuata
mkumbo,” anasema.
Anasema
badala ya kulalamika kukosa ajira, ni muhimu vijana wakafanya kazi kwa
kujitolea kwenye mashirika au kampuni, ili kupata uzoefu na maarifa zaidi.
Anasema
tangu alipojiajiri mwaka 2021, amefanikiwa kufundisha zaidi ya wakulima 2,000
wakiwamo aliowapa huduma bila malipo.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni