Jumamosi, 13 Aprili 2026 · Dar es Salaam, Tanzania
kijijichetumedia.com
Kijiji cha Habari Media
Kijiji cha Habari Media Simulizi za Mageuzi · SDGs · Tanzania
LEO
Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •    Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •   

Alhamisi, 11 Desemba 2025

Mwongozo rahisi wa kilimo cha celery nyumbani

 


Celery ni moja ya mboga zinazopendwa kwa ladha yake nzuri na matumizi mengi jikoni.

Hata hivyo, watu wengi hudhani kuwa inahitaji utaalamu na shamba kubwa ili kuikuza. Ukweli ni kwamba, unaweza kulima celery hata kwenye chupa ya plastiki ukitumia nafasi ndogo tu uliyonayo nyumbani. Mwongozo huu unakuelekeza hatua kwa hatua jinsi ya kuandaa chupa, kupanda, kutunza na hatimaye kuvuna celery safi bila kutumia gharama kubwa.

Cerely inapendwa kutokana na utajiri wake mkubwa wa virutubisho na hutumika sana jikoni kwa kuongeza ladha na harufu kwenye vyakula mbalimbali.

Habari njema ni kwamba celery inaweza kulimwa katika mazingira madogo, ikiwemo kwenye chupa za plastiki na ndio maana leo nakuletea mwongozo huu unakuelekeza jinsi ya kulima celery ukiwa nyumbani bila gharama kubwa.

Ili kuanza, andaa chupa kubwa ya plastiki yenye ujazo wa lita mbili ni bora zaidi.

Udongo wenye rutuba na wenye mbolea asilia, masalia ya shina la celery au mbegu zake, maji na eneo lenye mwanga wa jua.

DONDOO

Kata sehemu ya juu ya chupa, takribani sentimita 15–20 kutoka chini, ili kupata nafasi ya kutosha kwa mizizi.

Tengeneza mashimo madogo chini ya chupa ili kuruhusu maji kupita na kuzuia kuoza kwa mizizi.

Ikiwa unataka mfumo wa kujimwagilia yenyewe, kata chupa katikati na geuza sehemu ya juu kuwa kifuniko chenye umbo la kinyunyuzi (funnel), kinachoingia kwenye sehemu ya chini. Tumia kitambaa chepesi kama utambi, kuvuta maji kutoka kwenye sehemu ya chini kwenda juu.

Jaza udongo wenye rutuba uliochanganywa na samadi kwenye chupa na hakikisha udongo una uwezo mzuri wa kupitisha maji.

Kama unatumia masalia ya shina la celery, chukua sehemu ya chini ya shina (root base), lililobaki baada ya kukata majani. Liweke juu ya udongo kwa kulibonyeza kidogo kisha funika kwa udongo kiasi.

Kwa mbegu, pandikiza mbegu juu ya udongo, kisha nyunyizia udongo mlaini kuzifunika kisha mwagilia maji kiasi cha kutosha ili kufanya udongo uwe na unyevu wa wastani. Celery inapenda udongo wenye unyevu muda wote, hivyo huna budi kuhakikisha hayakauki japokuwa unapaswa kuepuka maji mengi kupita kiasi ili mizizi isioze.

Weka chupa kwenye eneo lenye mwanga wa jua wa angalau masaa 4–6 kwa siku.

Ikiwa jua ni kali sana, weka chupa sehemu ambayo hupata mwanga wa jua usio wa moja kwa moja.

Jambo muhimu la kuzingatia ni kuangalia unyevu wa udongo kila siku, hasa katika vipindi vya joto.

Ikiwa mmea unaonekana dhaifu, ongeza mbolea ya maji (liquid fertilizer) mara moja kwa wiki au mbili.

Celery hukomaa baada ya wiki 10–12 kulingana na hali ya hewa.

Unaweza kuvuna majani hatua kwa hatua au kusubiri mmea ukomae kisha uvune shina lote.

Mara baada ya kuvuna, unaweza kuendelea kutumia masalia ya shina kuotesha mmea mwingine ndani ya chupa hiyo hiyo.

Kulima celery kwenye chupa ya plastiki ni njia rahisi, ya gharama nafuu na rafiki kwa mazingira. Hakuhitaji bustani kubwa wala vifaa vya gharama. Kwa kufuata hatua zilizotajwa, unaweza kufurahia celery safi na yenye ladha nzuri kutoka kwenye bustani yako ndogo ya nyumbani.

Ni kilimo rahisi kinachoweza kufanyika mjini na vijijini hasa kwa watu wenye eneo dogo.


PICHA ZOTE NA PINTEREST

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni