TUNAPOELEKEA kuadhimisha sikukuu ya Krismasi ambayo
Wakristo duniani kote, wanaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, ambaye wanaamini
kwamba ni msingi wa imani yao, pambo ndiyo tafsiri halisi ya sherehe hiyo.
Kuanzia kwenye maduka, ofisi za umma na binafsi, nyumba
na sehemu za starehe, hakuna iliyobaki bila kupambwa kuashiria sikukuu hii. Upekee
wa mapambo unaoamsha shamrashamra za watu wengi, unatokana na kwamba sherehe
hizi zinaambatana na mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Hii ndio maana kwa ujumla kila familia kunakuwa na
hali ya hewa ya furaha ya kumaliza mwaka.
Kwanza ni muhimu kuelewa kwamba mapambo ya Krismasi si
lazima yawe magumu ili yaonekane ya kifahari. Unaweza kutumia vitu rahisi na
kubadilisha mwonekano wa nyumba yako mara moja.
Kuanzia mti wa Krismasi, taa za rangi, mishumaa, maua
ya bandia hadi picha na maandishi ya heri ya sikukuu, kila pambo hubeba ujumbe
wake.
Wataalamu wa mapambo wanasema kuwa ubunifu na matumizi
sahihi ya rasilimali zilizopo vinaweza kuleta matokeo bora zaidi. Vifaa rahisi
kama karatasi za kufungashia zawadi, pine cones, vifuniko vya chupa, pipi na
hata nguo zilizochakaa vinaweza kutumika kutengeneza mapambo ya kipekee ya
kujitengenezea (DIY).
Mbinu hii si tu huokoa gharama, bali pia husaidia
kulinda mazingira kwa kupunguza taka na kuhamasisha matumizi ya vitu vilivyopo
badala ya kununua vipya.
Mapambo ya Krismasi pia ni fursa ya kuimarisha
mshikamano wa kifamilia. Kutengeneza mapambo pamoja na watoto na wanafamilia
wengine huleta furaha, hujenga kumbukumbu za kudumu na kuwafundisha watoto
umuhimu wa ubunifu, uvumilivu na kushirikiana.
Iwe ni nyumba kubwa, chumba cha kupanga, ofisi, darasa
au duka, mapambo ya Krismasi yanaweza kubuniwa kulingana na nafasi iliyopo.
Mapambo madogo kama mishumaa, mapambo ya ukutani au taa ndogo yanaweza kutoa
mvuto mkubwa hata katika maeneo yenye nafasi finyu.
Kwa upande wa wafanyabiashara, mapambo ya Krismasi
husaidia kuvutia wateja, kuongeza mauzo na kuleta hali ya ukarimu inayochochea
biashara katika msimu wa sikukuu.
Mapambo ya Krismasi ni zaidi ya urembo; ni lugha ya
furaha, matumaini na upendo. Kwa kutumia ubunifu, ushirikiano wa familia na
rasilimali zilizopo, kila mtu anaweza kufurahia mandhari ya Krismasi bila
kujali bajeti au ukubwa wa nafasi.
Unaweza kutumia 'vase' za maua kama zinavyoonekana pichani juu kuweka mapambo ya Krismasi ili kubadilisha mwonekano na kuleta mvuto wa sikukuu.
Picha: PINTEREST



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni