KATIKA dunia ya leo, changamoto za afya kama uchovu wa
kudumu, msongo wa mawazo, matatizo ya kumbukumbu na maumivu ya mifupa zimekuwa
sehemu ya maisha ya watu wengi.
Wataalamu wa afya wanabainisha kuwa chanzo kikuu cha
matatizo haya si umri pekee, bali ni lishe duni isiyo na virutubisho muhimu.
Makala hii inaeleza umuhimu wa protini, vitamini D, vyakula vya afya ya ubongo
na magnesiamu, kwa kuzingatia vyakula vinavyopatikana kwa urahisi hapa
Tanzania.
Protini ni nguzo kuu ya ujenzi wa misuli, ngozi, damu
na homoni. Upungufu wa protini husababisha kudhoofika kwa misuli, kinga hafifu
na uchovu wa haraka.
Vyakula vyenye protini kwa wingi:
Samaki (dagaa, sato, sangara)
Mayai
Maharagwe, dengu na choroko
Kuku na nyama ya ng’ombe
Karanga, njugu na soya
Kwa familia za Kitanzania, vyakula hivi vinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu, hasa samaki wadogo kama dagaa na mikunde.
Vitamini D: Msingi wa Mifupa Imara
Vitamini D husaidia mwili kunyonya kalsiamu na
kuimarisha mifupa na meno. Upungufu wake huongeza hatari ya maumivu ya mifupa
na udhaifu wa mwili.
Chanzo cha Vitamini D ni mwanga wa jua (dakika 15–30
kila siku).
Samaki wenye mafuta mengi
Mayai (hasa kiini)
Maziwa yaliyoongezwa vitamini D
Uyoga
Kwa mazingira ya Tanzania yenye jua la kutosha,
wananchi wanahimizwa kutumia mwanga wa asili sambamba na lishe sahihi.
Vyakula kwa afya ya ubongo
Ubongo unahitaji lishe maalumu, ili kuimarisha
kumbukumbu, umakini na kupunguza hatari ya magonjwa ya mfumo wa neva.
Samaki wenye mafuta mengi.
Karanga na mbegu (maboga, ufuta, alizeti)
Mboga za majani ya kijani kibichi
Mayai
Parachichi
Lishe hii husaidia watoto shuleni, watu wazima kazini
na wazee kudumisha afya ya akili.
Magnesiamu: Madini Muhimu kwa msongo na usingizi
Magnesiamu husaidia misuli kufanya kazi vizuri,
kupunguza msongo wa mawazo na kuboresha usingizi.
Vyakula vyenye magnesiamu:
Mbegu za maboga
Maharagwe na dengu
Mboga za majani
Ndizi
Nafaka zisizokobolewa
Upungufu wa magnesiamu husababisha misuli kukakamaa,
usingizi hafifu na wasiwasi.
Kama ulivyoona aina za vyakula hapo juu, ni wazi
kwamba lishe bora haihitaji vyakula vya gharama kubwa. Kwa kupanga mlo unaojumuisha
ugali wa dona, wali wa kahawia, samaki, mikunde, mboga za majani na matunda,
familia inaweza kupata virutubisho vyote muhimu.
Kwa lugha nyingine, afya nzuri huanzia jikoni. Lishe
bora yenye protini, vitamini D, magnesiamu na virutubisho vya afya ya ubongo ni
uwekezaji wa maisha marefu na yenye ubora.
Je, familia yako inazingatia lishe bora? Endelea
kufuatilia Kijiji Chetu Media kwa makala zaidi za afya, lishe na maisha bora.
RATIBA YA CHAKULA
Nimekuandalia ratiba rahisi ya chakula, ambayo unaweza
kuitumia nyumbani na hususani wakati huu wa likizo.
Asubuhi unaweza kuanza na kifungua kinywa kwa uji wa
dona wenye maziwa, mayai ya kuchemsha na ndizi.
Mchana ukajipatia ugali wa dona, maharagwe yaliyoungwa
nazi, mchicha na juisi fresh (huu ni msimu wa matunda); au tunda zima, embe,
nanasi, ndizi mbivu au tikiti. Inategemea ulipo na tunda linalopatikana kwa
urahisi.
Jioni unaweza kuandaa wali, samaki wa kukaanga (dagaa
au sato), mboga za majani.
Siku nyingine unaweza kufungua kinywa na mkate wa
ngano nzima, siagi ya karanga, chai ya maziwa; mchana ukala wali na kuku wa
kuungwa, kisamvu na tunda lolote halafu jioni ukajipatia viazi vitamu au mihogo,
mayai, parachichi na mboga za majani.
Wakati mwingine asubuhi unaweza kuandaa breakfast ya mayai
ya kukaanga kwa mafuta kidogo, chai ya rangi au ya maziwa, matunda (tikiti au
papai); halafu mchana ukajiramba ugali kwa samaki wa mchizi na matembele na
usiku ukapika zako ndizi, maharage na bamia pamoja na biringanya.
Siku nyingine unaweza kupata kifungua kinywa miongoni
mwa nilivyotaja hapo juu, halafu mchana ukala wali nyama ya ng’ombe na
mboga za majani.
Unaweza pia kula mtindi, karanga, korosho au almondi
wakati wa mlo au unapohisi njaa.
Aidha, badala ya maharage unaweza kupika kunde, njugu,
choroko au aina nyingine ya mikunde.
Katika makala haya, nimetaja baadhi tu ya vyakula, bila shaka mahali ulipo unaweza kupata bora na chaguo linalofaa zaidi.
Kijiji Chetu Media
inaendelea kuhimiza jamii kuchagua chakula bora kwa afya ya sasa na ya vizazi
vijavyo.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni