Jumamosi, 13 Aprili 2026 · Dar es Salaam, Tanzania
kijijichetumedia.com
Kijiji cha Habari Media
Kijiji cha Habari Media Simulizi za Mageuzi · SDGs · Tanzania
LEO
Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •    Fugakuku Business Solution yafunza wafugaji 2,000+ Tanzania — Soma simulizi yake hapa    •   

Jumatatu, 18 Agosti 2025

Jinsi ya kutengeneza bustani ya maua inayotumia maji kidogo

MAWE, uchaguzi makini wa mimea, mbinu bora za umwagiliaji na usimamizi mzuri wa udongo, ni mambo yanayoweza kusaidia ndoto yako ya kuwa na bustani ya maua nyumbani.

Mbinu hizi ni kwa wale ambao wanapenda bustani, lakini hawana chanzo kizuri cha maji au pengine gharama za kulipia maji kwa ajili ya bustani ya maua, ni kubwa.

Kama uko katika hali niliyoieleza hapo juu, soma makala haya mpaka mwisho.

Mosi, ni vyema ukafahamu kwamba ipo mimea ambayo inatumia maji kidogo na inahimili jua au hali ya ukame. Yapo yanayoweza kuchanua mwaka mzima na pia yapo yasiyochanua. Ni muhimu kufahamu aina unayotaka.

Baadhi ya maua haya ni jesus, lavenda, kitenge, fuhsia, alstromeria, kalanchoe, mandevile, jasmine, hibiscus, american palm (na aina nyingine za palm), na nyasi aina ya buffalo (zile zenye majani mapana kidogo).

Aina hizi pamoja na mengineyo, yanaweza kumwagiliwa mara moja kwa wiki, yana sifa kubwa ya pekee ambayo ni kutodhuriwa kirahisi na wadudu, hayavamiwi na mchwa na yanatumia maji, mbolea na virutubisho vingine kwa kiasi kidogo sana.

Baada ya kuchagua aina ya maua, tengeneza ratiba ya kuyamwagilia. Hapa inashauriwa ufunge mfumo wa umwagiliaji wa matone, ili maji kidogo uliyonayo yafike kwenye mmea wako bila kupotea.

Mfumo huu utakupunguza matumizi ya maji kwa kiasi kikubwa, huku ukiendelea kufurahia mandhari ya kupendeza.

DONDOO MUHIMU

·      Chagua mimea inayostahimili ukame hasa miti, maua ya asili na nyasi za mapambo na kuipanda kulingana namna eneo lako lilivyo.

·      Zingatia ukubwa na umri wa mmea, mimea yenye mizizi mirefu huwa na uwezo mkubwa wa kustahimili ukame kuliko miche michanga.

·      Fanya usimamizi makini wa udongo, kwa kuongeza samadi, ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi unyevu na kusaidia mifereji ya maji na pia unaweza kutandaza majani makavu kuzunguka mmea, ili kutunza unyevu.

·      Ongeza sehemu za kupita, weka mawe au kokoto katika baadhi ya maeneo, ili kupunguza mimea na hivyo kupunguza matumizi ya maji. Mawe huongeza uzuri wa asili.

·      Unaweza kupanda lavenda, jesus, jasmini, rosemary na minti, ambayo yanahitaji matunzo kidogo na inastahimili ukame.

·       Mwagilia mapema asubuhi au jioni jua likiwa limezama, ili kupunguza upotevu wa maji.

·       Ondoa magugu mara kwa mara kwa kuwa kuwapo kwa mimea vamizi bustanini kwako, kunasababisha magugu na maua yako kugombea maji pamoja na virutubisho vingine.

·       Kwenye mawe, tumia yenye ukubwa tofauti ili kuongeza mvuto asilia.

Aidha, pamoja na kwamba maua haya yanahimili jua, ukiyaweka kivulini yanafanya vizuri zaidi, kwa hiyo nakushauri pamoja na uwezo wake mkubwa wa kutumia maji kidogo, unaweza kupanda miti kadhaa, ili kutengeneza kivuli kwa ajili ya maua yako.

Picha zote na Pinterest.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni