KILA nyumba ina harufu yake ya kipekee; wakati mwingine ni nzuri na wakati mwingine si ya kupendeza. Kwa wale wanasumbuka kutengeneza nyumba yenye harufu nzuri, suluhisho lipo.
Wataalamu wa usafi wa mazingira ya nyumbani, wanashauri
mbinu rahisi na nafuu zinazoweza kubadili nyumba kuwa mahali panapovutia kwa
harufu nzuri wakati wote.
Usafi ndiyo nguzo
Kwanza, jambo la msingi ni kuhakikisha nyumba
inasafishwa mara kwa mara, kwa kupiga deki, kufuta vumbi na kuondoa vitu
visivyotumika. Bila kufanya hivi, harufu mbaya inaweza kuendelea kujitokeza.
Ili kupata matokeo mazuri, wakati wa usafi ni muhimu
kuzingatia eneo lenye zulia, mapazia na vitambaa; kwa kuhakikisha yanafuliwa
mara kwa mara ili kuepuka kukusanya vumbi.
Pia, eneo la taka, hili ndilo chanzo kikuu cha harufu
mbaya nyumbani, hivyo hakikisha ni safi kila wakati.
Friji, ikiwezekana safisha angalau mara moja kwa wiki,
kuondoa mabaki yanayosababisha harufu.
Nguo, inashauriwa kwamba usihifadhi nguo chafu kwa
muda mrefu; zifue na hakikisha zimekauka vizuri.
Pili, weka mimea kama rosemary, mint au maua kama
snake plant ndani. Hii inavutia na pia inasaidia kusafisha hewa na kuondoa
vichafuzi vinavyosababisha harufu. Aidha, maua kama yasmini, waridi au chani
huongeza mvuto wa harufu safi nyumbani.
Tatu, tumia air freshener ya asilia. Unaweza
kuchanganya maji na mafuta ya lavender na limao, na kunyunyiza (spray), ndani ya
nyumba kila siku.
Pia, unaweza kuchemsha maganda ya chungwa, mdalasini
au majani kavu ya maua kupata harufu ya asili.
Mbinu nyingine ni kutumia baking soda na siki
(vinegar), kuondoa unyevu na harufu mbaya. Siki pia ni dawa ya kusafisha na
kuua vijidudu.
Mbinu za nyongeza
Ni vyema kuwa na utaratibu wa kufungua madirisha na
milango kila asubuhi, ili kuruhusu hewa safi na mwanga wa jua kuzunguka. Unaweza
pia kutumia mishumaa yenye harufu nzuri kama ya lavenda, ua rose au matunda. Harufu
hizi laini zinatajwa kuongeza mandhari ya kustarehesha hasa wakati wa baridi.
Tumia pia mchanganyiko wa maua na majani yaliyokaushwa
na kuyaweka kabatini au kwenye chumba cha kulala, kuongeza harufu nzuri.
Inaweza pia kutumia vifaa vya kusambaza harufu
(diffusers), kwa ajili ya udi na manukato mengine; yakiwamo ya kupachika
ukutani.
Eneo lingine la kuzingatia sana ni usafi wa choo na
bafu. Hakikisha sakafu na taulo zinakauka vizuri, ili kuepuka unyevu
unaosababisha ukungu na harufu.
Wataalamu wanashauri kwamba ni vizuri ukaweka utaratibu wa kufanya usafi wa kina (deep cleaning), angalau mara moja kila baada ya miezi mitatu. Hii itafanya nyumba nzima kuwa safi kwa muda mrefu.
Njia za ziada za gharama nafuu
Weka bakuli la kahawa, mkaa au siki kwenye vyumba
tofauti husaidia kufyonza harufu mbaya mara moja.
Kwa kifupi, harufu ya nyumba huathiri hisia za wenyeji
na wageni. Nyumba safi, yenye harufu ya kupendeza, haileti tu faraja bali pia
hufanya mwenyeji ahisi fahari.
Unaweza kuchoma karafuu, ganda la limau au chungwa, kuleta harufu asilia.
Picha zote na PINTEREST.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni